Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu
Ufunuo 6
Mwana-Kondoo afungua mihuri saba
Nikaangalia Mwana-Kondoo alipofungua ule muhuri wa kwanza miongoni mwa mihuri saba. Ndipo nikasikia mmoja wa wale viumbe wanne wenye uhai akisema kwa sauti kama ya radi: “Njoo!” Nikatazama, na hapo mbele yangu palikuwa na farasi mweupe! Yeye aliyempanda alikuwa na upinde, naye akapewa taji, akampanda akatoka akiwa kama mshindi aelekeaye katika kushinda.
Alipouvunja ule muhuri wa pili, nikamsikia yule kiumbe wa pili mwenye uhai akisema, “Njoo!” Ndipo akatokea farasi mwingine mwekundu sana. Yeye aliyempanda akapewa uwezo wa kuondoa amani duniani na kuwafanya watu wauane. Yeye akapewa upanga mkubwa.
Mwana-kondoo alipouvunja ule muhuri wa tatu, nikamsikia yule kiumbe wa tatu mwenye uhai akisema, “Njoo!” Nikatazama, na mbele yangu palikuwa na farasi mweusi! Yeye aliyempanda alikuwa na mizani mkononi mwake. Ndipo nikasikia kile kilichokuwa kama sauti katikati ya wale viumbe wanne wenye uhai ikisema, “Kipimo kimoja1 cha ngano kwa mshahara wa kibarua wa siku moja2, na vipimo vitatu vya shayiri kwa mshahara wa kibarua cha siku moja. Lakini usiharibu mafuta wala divai!”
Alipouvunja ule muhuri wa nne, nikasikia sauti ya yule kiumbe wa nne mwenye uhai ikisema, “Njoo!” Nikatazama, na hapo mbele yangu palikuwa na farasi mwenye rangi ya kijivujivu! Yeye aliyempanda aliitwa Mauti, naye Kuzimu3 alikuwa akimfuata nyuma yake kwa karibu. Wakapewa mamlaka juu ya robo ya dunia, kuua kwa upanga, njaa, tauni na kwa wanyama wakali wa dunia.
Mwana-kondoo alipouvunja ule muhuri wa tano, nikaona chini ya madhabahu, roho za wale waliochinjwa kwa ajili ya neno la Mungu na kwa ajili ya ushuhuda walioutunza. Wakalia kwa sauti kuu, wakasema, “Hata lini, Ee Bwana Mungu Mwenyezi, uliye mtakatifu na mwaminifu, hutawahukumu na kulipiza kisasi kwa watu wanaoishi duniani kwa ajili ya damu yetu?” Kisha kila mmoja wao akapewa joho jeupe na wakaambiwa wangoje kwa muda kidogo zaidi, hadi idadi ya ndugu zao na watumishi wenzao watakaouawa kama wao walivyouawa, itakapotimia.
Nikatazama alipouvunja ule muhuri wa sita. Pakatokea tetemeko kuu la ardhi, na jua likawa jeusi kama gunia lililotengenezwa kwa singa za mbuzi, na mwezi wote ukawa mwekundu kama damu. Nyota zilizo angani zikaanguka ardhini kama vile matunda ya mtini yasiyokomaa yaangukavyo wakati mti wake unapotikiswa na upepo mkali. Anga ikatoweka kama vile karatasi isokotwavyo, na kila mlima na kila kisiwa kikaondolewa mahali pake.
Ndipo wafalme wa dunia, wakuu wote, majemadari, matajiri, wenye nguvu na kila mtu, mtumwa na mtu huru, wakajificha katika mapango na kwenye miamba ya milima. Wakaiita milima na miamba wakisema, “Tuangukieni, mkatufiche na uso wake yeye aliyeketi kwenye kile kiti cha enzi, na mkatuepushe na ghadhabu ya Mwana-Kondoo! Kwa maana siku ile kuu ya ghadhabu yao imewadia. Je, ni nani awezaye kustahimili?”
Source notes (3)
- Footnote Ni kama lita moja.
- Footnote Sawa na dinari moja.
- Footnote Kuzimu kwa Kiyunani ni Hades , yaani mahali pa wafu.
Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu. Copyright © 2018, 2024 Biblica, Inc. Licensed under CC BY-SA 4.0. “Biblica” ni alama ya biashara iliyosajiliwa katika United States Patent and Trademark Office (ofisi ya hataza na alama za biashara Marekani) na shirika la Biblica, Inc. Source: eBible.org. Typeset from the source files; no intended changes to scripture wording. BibleKenya is not endorsed by the rights holder.
Full source notice & licence · CC BY-SA 4.0 · SourceEdition imported 2026-10-25.