Skip to content
BibleKenya

Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu

Ufunuo 5

Kitabu na Mwana-Kondoo

Kisha nikaona katika mkono wake wa kuume wa yule aliyeketi kwenye kile kiti cha enzi, kitabu kilichoandikwa ndani na nje, kikiwa kimefungwa kwa mihuri saba. Nami nikamwona malaika mwenye nguvu akitangaza kwa sauti kuu, “Ni nani anayestahili kuivunja hiyo mihuri na kukifungua kitabu?” Lakini hapakuwa na yeyote mbinguni wala duniani au chini ya dunia aliyeweza kukifungua hicho kitabu, wala hata kutazama ndani yake. Nikalia sana kwa sababu hakuonekana yeyote anayestahili kukifungua hicho kitabu wala kutazama ndani yake. Kisha, mmoja wa wale wazee akaniambia, “Usilie! Tazama, Simba wa kabila la Yuda, wa Uzao wa Daudi, ameshinda. Yeye ndiye anayeweza kukifungua hicho kitabu na kuvunja mihuri yake saba.”

Ndipo nikaona katikati ya kile kiti cha enzi na wale viumbe wenye uhai wanne, na katikati ya wale wazee, Mwana-Kondoo amesimama, akiwa kama amechinjwa. Alikuwa na pembe saba na macho saba, ambazo ndizo zile Roho saba1 za Mungu zilizotumwa duniani pote. Huyo Mwana-Kondoo akaja na kukitwaa kile kitabu kutoka mkono wa kuume wa yule aliyeketi kwenye kile kiti cha enzi. Alipokwisha kukitwaa kile kitabu, wale viumbe wenye uhai wanne pamoja na wale wazee ishirini na wanne wakaanguka mbele ya yule Mwana-Kondoo. Kila mmoja wao alikuwa na kinubi, nao walikuwa wameshika mabakuli ya dhahabu yaliyojaa uvumba, ambayo ni maombi ya watakatifu. Nao wakaimba wimbo mpya, wakisema:

“Wewe unastahili kukitwaa kitabu

na kuivunja mihuri yake,

kwa sababu ulichinjwa,

na kwa damu yako ukamnunulia Mungu

watu kutoka kila kabila, kila lugha,

kila jamaa na kila taifa.

Wewe umewafanya hawa wawe ufalme na makuhani

wa kumtumikia Mungu wetu,

nao watatawala duniani.”

Kisha nikatazama, nikasikia sauti za malaika wengi wakiwa wamekizunguka kile kiti cha enzi, pamoja na wale viumbe wenye uhai wanne na wale wazee ishirini na wanne. Idadi yao ilikuwa kumi elfu mara kumi elfu na maelfu ya maelfu. Nao waliimba kwa sauti kuu, wakisema:

“Anastahili Mwana-Kondoo, yeye aliyechinjwa,

kupokea uweza na utajiri na hekima na nguvu

na heshima na utukufu na sifa!”

Kisha nikasikia kila kiumbe mbinguni na duniani, chini ya nchi, na baharini, na vyote vilivyomo, vikiimba:

“Sifa na heshima na utukufu na uweza

ni vyake yeye aliyeketi juu ya hicho kiti cha enzi,

na kwa Mwana-Kondoo,

milele na milele!”

Wale viumbe wenye uhai wanne wakasema, “Amen!” Nao wale wazee wakaanguka kifudifudi wakaabudu.

Source notes (1)
  1. Footnote Roho saba za Mwenyezi Mungu hapa inamaanisha Roho wa Mungu katika ukamilifu wa utendaji wake.

Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu. Copyright © 2018, 2024 Biblica, Inc. Licensed under CC BY-SA 4.0. “Biblica” ni alama ya biashara iliyosajiliwa katika United States Patent and Trademark Office (ofisi ya hataza na alama za biashara Marekani) na shirika la Biblica, Inc. Source: eBible.org. Typeset from the source files; no intended changes to scripture wording. BibleKenya is not endorsed by the rights holder.

Full source notice & licence · CC BY-SA 4.0 · SourceEdition imported 2026-10-25.

BibleKenya

Reader settings

Theme
Font
Alignment
Reading width

Saved in this browser and used offline too. Press ? for keyboard shortcuts.