Skip to content
BibleKenya

Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu

Zaburi 80

Maombi kwa ajili ya kuponywa kwa taifa

Kwa mwimbishaji. Mtindo wa “Yungiyungi za Agano”. Zaburi ya Asafu.

Ee Mchungaji wa Israeli tusikie,

wewe umwongozaye Yusufu kama kundi;

wewe uketiye kwenye kiti cha enzi

katikati ya makerubi, angaza

mbele ya Efraimu, Benyamini na Manase.

Uamshe nguvu zako,

uje utuokoe.

Ee Mungu, uturejeshe,

utuangazie uso wako,

ili tuweze kuokolewa.

Ee Bwana Mwenyezi Mungu,

Mungu wa majeshi ya mbinguni,

hata lini hasira yako itawaka

dhidi ya maombi ya watu wako?

Umewalisha kwa mkate wa machozi,

umewafanya wanywe machozi bakuli tele.

Tumekuwa chanzo cha ugomvi kwa majirani zetu,

na adui zetu wanatudhihaki.

Ee Mungu wa majeshi ya mbinguni, uturejeshe;

utuangazie uso wako,

nasi tuweze kuokolewa.

Ulileta mzabibu kutoka Misri,

ukawafukuza mataifa, ukaupanda.

Uliandaa shamba kwa ajili yake,

mizizi ikawa imara, ukajaza nchi.

Milima ilifunikwa kwa kivuli chake,

matawi yake yakafunika mierezi mikubwa.

Matawi yake yalienea hadi Baharini1,

machipukizi yake hadi kwenye Mto2.

Mbona umebomoa kuta zake

ili wote wapitao karibu

wazichume zabibu zake?

Nguruwe mwitu wanauharibu,

na viumbe wa kondeni hujilisha humo.

Turudie, Ee Mungu wa majeshi ya mbinguni!

Tazama chini kutoka mbinguni na uone!

Linda mzabibu huu,

mche ulioupanda kwa mkono wako wa kuume,

mwana uliyemlea

kwa ajili yako mwenyewe.

Mzabibu wako umekatwa, umechomwa moto,

unapowakemea, watu wako huangamia.

Mkono wako na utulie juu ya mtu aliye katika mkono wako wa kuume,

mwana wa mtu uliyemlea kwa ajili yako mwenyewe.

Ndipo hatutakuacha tena,

utuhuishe, nasi tutaliitia jina lako.

Ee Bwana Mwenyezi Mungu,

Mungu wa majeshi ya mbinguni, uturejeshe;

utuangazie uso wako,

ili tuweze kuokolewa.

Source notes (2)
  1. Footnote pengine ni Bahari ya Mediterania
  2. Footnote yaani Mto Frati

Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu. Copyright © 2018, 2024 Biblica, Inc. Licensed under CC BY-SA 4.0. “Biblica” ni alama ya biashara iliyosajiliwa katika United States Patent and Trademark Office (ofisi ya hataza na alama za biashara Marekani) na shirika la Biblica, Inc. Source: eBible.org. Typeset from the source files; no intended changes to scripture wording. BibleKenya is not endorsed by the rights holder.

Full source notice & licence · CC BY-SA 4.0 · SourceEdition imported 2026-10-25.

BibleKenya

Reader settings

Theme
Font
Alignment
Reading width

Saved in this browser and used offline too. Press ? for keyboard shortcuts.