Skip to content
BibleKenya

Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu

Zaburi 79

Maombi kwa ajili ya wokovu wa taifa

Zaburi ya Asafu.

Ee Mungu, mataifa yameuvamia urithi wako,

wamelinajisi Hekalu lako takatifu,

wameifanya Yerusalemu kuwa magofu.

Wametoa maiti za watumishi

kuwa chakula cha ndege wa angani

na nyama ya watakatifu wako

kwa wanyama wa nchi.

Wamemwaga damu kama maji

kuzunguka Yerusalemu yote,

wala hakuna yeyote wa kuwazika.

Tumekuwa kitu cha aibu kwa majirani zetu,

cha dharau na mzaha kwa wale wanaotuzunguka.

Hata lini, Ee Mwenyezi Mungu? Je, wewe utakasirika milele?

Wivu wako utawaka kama moto hadi lini?

Mwaga ghadhabu yako kwa mataifa yasiyokukubali,

juu ya falme za hao wasioliitia jina lako,

kwa maana wamemrarua Yakobo

na kuharibu nchi ya makao yake.

Usituhesabie dhambi za baba zetu,

huruma yako na itujie hima,

kwa maana tu wahitaji mno.

Ee Mungu Mwokozi wetu, utusaidie,

kwa ajili ya utukufu wa jina lako;

tuokoe na kutusamehe dhambi zetu

kwa ajili ya jina lako.

Kwa nini mataifa waseme,

“Yuko wapi Mungu wenu?”

Mbele ya macho yetu,

dhihirisha kati ya mataifa

kwamba unalipiza kisasi damu iliyomwagwa

ya watumishi wako.

Kilio cha huzuni cha wafungwa kifike mbele zako;

kwa nguvu za mkono wako

hifadhi wale waliohukumiwa kufa.

Walipize majirani zetu mara saba

aibu walizovurumisha kwako, Ee Bwana.

Ndipo sisi watu wako, kondoo wa malisho yako,

tutakusifu milele;

tutasimulia sifa zako

kizazi hadi kizazi.

Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu. Copyright © 2018, 2024 Biblica, Inc. Licensed under CC BY-SA 4.0. “Biblica” ni alama ya biashara iliyosajiliwa katika United States Patent and Trademark Office (ofisi ya hataza na alama za biashara Marekani) na shirika la Biblica, Inc. Source: eBible.org. Typeset from the source files; no intended changes to scripture wording. BibleKenya is not endorsed by the rights holder.

Full source notice & licence · CC BY-SA 4.0 · SourceEdition imported 2026-10-25.

BibleKenya

Reader settings

Theme
Font
Alignment
Reading width

Saved in this browser and used offline too. Press ? for keyboard shortcuts.