Skip to content
BibleKenya

Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu

Zaburi 30

Maombi ya shukrani

Utenzi wa kuweka wakfu hekalu. Zaburi ya Daudi.

Nitakutukuza wewe, Ee Mwenyezi Mungu,

kwa kuwa umeniinua kutoka vilindi,

na hukuacha adui zangu

washangilie juu yangu.

Ee Mwenyezi Mungu, Mungu wangu, nilikuita unisaidie

na wewe umeniponya.

Ee Mwenyezi Mungu, umenitoa Kuzimu1,

umeniokoa nisishuke kwenye shimo la mauti.

Mwimbieni Mwenyezi Mungu, enyi watakatifu wake;

lisifuni jina lake takatifu.

Kwa maana hasira yake ni ya muda mfupi,

bali upendo wake hudumu siku zote.

Inawezekana kilio kiwepo usiku kucha,

lakini furaha huja asubuhi.

Nilipofanikiwa nilisema,

“Sitatikiswa kamwe.”

Ee Mwenyezi Mungu, uliponijalia,

uliuimarisha mlima wangu,

lakini ulipouficha uso wako

nilifadhaika.

Kwako wewe, Ee Mwenyezi Mungu, niliita,

niliomba rehema kwa Bwana:

“Kuna faida gani katika kuangamia kwangu,

katika kushuka kwangu shimoni?

Je, mavumbi yatakusifu?

Je, yatatangaza uaminifu wako?

Ee Mwenyezi Mungu, unisikie na kunihurumia;

Ee Mwenyezi Mungu, uwe msaada wangu.”

Uligeuza maombolezo yangu kuwa kucheza,

ulinivua gunia ukanivika shangwe,

ili moyo wangu uweze kukusifu na usikae kimya.

Ee Mwenyezi Mungu, Mungu wangu, nitakushukuru milele.

Source notes (1)
  1. Footnote Kuzimu kwa Kiebrania ni Sheol , yaani Shimo lisilo na mwisho.

Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu. Copyright © 2018, 2024 Biblica, Inc. Licensed under CC BY-SA 4.0. “Biblica” ni alama ya biashara iliyosajiliwa katika United States Patent and Trademark Office (ofisi ya hataza na alama za biashara Marekani) na shirika la Biblica, Inc. Source: eBible.org. Typeset from the source files; no intended changes to scripture wording. BibleKenya is not endorsed by the rights holder.

Full source notice & licence · CC BY-SA 4.0 · SourceEdition imported 2026-10-25.

BibleKenya

Reader settings

Theme
Font
Alignment
Reading width

Saved in this browser and used offline too. Press ? for keyboard shortcuts.