Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu
Zaburi 17
Sala ya mtu asiye na hatia
Sala ya Daudi.
Sikia, Ee Mwenyezi Mungu, kusihi kwangu kwa haki,
sikiliza kilio changu.
Tega sikio kwa ombi langu,
halitoki katika midomo ya udanganyifu.
Hukumu yangu na itoke kwako,
macho yako na yaone yale yaliyo haki.
Ingawa unauchunguza moyo wangu na kunikagua usiku,
ingawa umenijaribu, hutaona chochote.
Nimeamua kwamba kinywa changu
hakitatenda dhambi.
Kuhusu matendo ya wanadamu:
kwa neno la midomo yako,
nimejiepusha na njia za wenye jeuri.
Hatua zangu zimeshikamana na njia zako;
nyayo zangu hazikuteleza.
Ee Mungu, ninakuita, kwa kuwa utanijibu,
nitegee sikio lako na usikie ombi langu.
Uoneshe ajabu ya upendo wako mkuu,
wewe unayeokoa kwa mkono wako wa kuume
wale wanaokukimbilia kutokana na adui zao.
Nilinde kama mboni ya jicho lako,
unifiche chini ya kivuli cha mabawa yako
kutokana na waovu wanaonishambulia,
kutokana na adui wauaji wanaonizunguka.
Huifunga mioyo yao iliyo migumu,
vinywa vyao hunena kwa majivuno.
Wamenifuatia nyayo zangu, sasa wamenizingira,
wakiwa macho, waniangushe chini.
Wamefanana na simba mwenye njaa anayewinda,
kama simba mkubwa anayenyemelea mafichoni.
Inuka, Ee Mwenyezi Mungu, pambana nao, uwaangushe,
niokoe kwa upanga wako kutoka kwa waovu.
Ee Mwenyezi Mungu, mkono wako uniokoe na watu kama hawa,
kutokana na watu wa ulimwengu huu
ambao fungu lao liko katika maisha haya.
Na wapate adhabu ya kuwatosha.
Watoto wao na wapate zaidi ya hayo,
hukumu na iendelee kwa watoto wa watoto wao.
Bali mimi nitauona uso wako katika haki;
niamkapo, nitaridhika kwa kuona sura yako.
Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu. Copyright © 2018, 2024 Biblica, Inc. Licensed under CC BY-SA 4.0. “Biblica” ni alama ya biashara iliyosajiliwa katika United States Patent and Trademark Office (ofisi ya hataza na alama za biashara Marekani) na shirika la Biblica, Inc. Source: eBible.org. Typeset from the source files; no intended changes to scripture wording. BibleKenya is not endorsed by the rights holder.
Full source notice & licence · CC BY-SA 4.0 · SourceEdition imported 2026-10-25.