Skip to content
BibleKenya

Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu

Zaburi 16

Sala ya matumaini

Utenzi wa Daudi.

Ee Mungu, uniweke salama,

kwa maana kwako nimekimbilia.

Nilimwambia Mwenyezi Mungu, “Wewe ndiwe Bwana wangu;

pasipo wewe sina jambo jema.”

Kuhusu watakatifu walio duniani,

hao ndio wenye fahari,

na ninapendezwa nao.

Huzuni itaongezeka kwa wale

wanaokimbilia miungu mingine.

Sitazimimina sadaka za damu kwa miungu kama hiyo,

au kutaja majina yao mdomoni mwangu.

Mwenyezi Mungu umeniwekea fungu langu na kikombe changu;

umeyafanya mambo yangu yote yawe salama.

Alama za mipaka zimeniangukia mahali pazuri,

hakika nimepata urithi mzuri.

Nitamsifu Mwenyezi Mungu ambaye hunishauri,

hata wakati wa usiku moyo wangu hunifundisha.

Nimemweka Mwenyezi Mungu mbele yangu daima.

Kwa sababu yuko mkono wangu wa kuume,

sitatikisika.

Kwa hiyo moyo wangu unafurahia,

na ulimi wangu unashangilia;

mwili wangu nao

utapumzika salama,

kwa maana hutaniacha Kuzimu1,

wala hutamwacha Mtakatifu Wako

kuona uharibifu.

Umenijulisha njia ya uzima;

utanijaza na furaha mbele zako,

pamoja na furaha ya milele

katika mkono wako wa kuume.

Source notes (1)
  1. Footnote Kuzimu kwa Kiebrania ni Sheol , yaani Shimo lisilo na mwisho.

Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu. Copyright © 2018, 2024 Biblica, Inc. Licensed under CC BY-SA 4.0. “Biblica” ni alama ya biashara iliyosajiliwa katika United States Patent and Trademark Office (ofisi ya hataza na alama za biashara Marekani) na shirika la Biblica, Inc. Source: eBible.org. Typeset from the source files; no intended changes to scripture wording. BibleKenya is not endorsed by the rights holder.

Full source notice & licence · CC BY-SA 4.0 · SourceEdition imported 2026-10-25.

BibleKenya

Reader settings

Theme
Font
Alignment
Reading width

Saved in this browser and used offline too. Press ? for keyboard shortcuts.