Skip to content
BibleKenya

Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu

Mithali 19

Afadhali mtu maskini ambaye mwenendo wake hauna lawama,

kuliko mpumbavu ambaye midomo yake imepotoka.

Sio vizuri kuwa na juhudi bila maarifa,

wala kufanya haraka na kuikosa njia.

Upumbavu wa mtu mwenyewe huharibu maisha yake

hata hivyo moyo wake humkasirikia Mwenyezi Mungu.

Mali huleta rafiki wengi,

bali rafiki wa mtu maskini humwacha.

Shahidi wa uongo hataacha kuadhibiwa,

naye amwagaye uongo hataachwa huru.

Wengi hujipendekeza kwa mtawala

na kila mmoja ni rafiki wa mtu atoaye zawadi.

Mtu maskini huepukwa na ndugu zake wote:

Je, rafiki zake watamkwepa kiasi gani!

Ingawa huwafuata kwa kuwasihi,

hawapatikani popote.

Yeye apataye hekima huipenda nafsi yake mwenyewe,

yeye ahifadhiye ufahamu hustawi.

Shahidi wa uongo hataacha kuadhibiwa,

naye amwagaye uongo ataangamia.

Haistahili mpumbavu kuishi katika anasa,

itakuwa vibaya kiasi gani

kwa mtumwa kuwatawala wakuu.

Hekima ya mtu humpa uvumilivu,

ni kwa utukufu wake kusamehe makosa.

Ghadhabu ya mfalme ni kama mngurumo wa simba,

bali wema wake ni kama umande juu ya nyasi.

Mwana mpumbavu ni maangamizi ya babaye,

naye mke mgomvi ni kama kutonatona kusikoisha.

Nyumba na mali hurithiwa kutoka kwa wazazi,

bali mke mwenye busara hutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Uvivu huleta usingizi mzito,

naye mtu mzembe huona njaa.

Yeye ambaye hutii mafundisho huulinda uhai wake,

bali yeye anayezidharau njia zake atakufa.

Yeye amhurumiaye maskini humkopesha Mwenyezi Mungu,

naye atamtuza kwa aliyotenda.

Mkanye mwanao, kwa maana kufanya hivyo kuna tumaini,

usiwe mshirika katika mauti yake.

Mtu mwenye kukasirika haraka ni lazima atapata adhabu yake,

kama utamwokoa, itakubidi kufanya hivyo tena.

Sikiliza mashauri na ukubali mafundisho,

nawe mwishoni utakuwa na hekima.

Kuna mipango mingi ndani ya moyo wa mtu,

lakini kusudi la Mwenyezi Mungu ndilo litakalosimama.

Lile mtu alionealo shauku ni upendo usio na mwisho,

afadhali kuwa maskini kuliko kuwa mwongo.

Kumcha Mwenyezi Mungu huongoza kwenye uzima,

kisha mtu hupumzika akiwa ameridhika,

bila kuguswa na shida.

Mtu mvivu hutumbukiza mkono wake kwenye sahani,

lakini hawezi hata kuupeleka kwenye kinywa chake!

Mpige mwenye mzaha, naye mjinga atajifunza busara,

mkemee mwenye ufahamu naye atapata maarifa.

Yeye amwibiaye baba yake na kumfukuza mama yake

ni mwana aletaye aibu na fedheha.

Mwanangu, ukiacha kusikiliza mafundisho,

utatangatanga mbali na maneno ya maarifa.

Shahidi mla rushwa hudhihaki hukumu

na kinywa cha mtu mwovu humeza ubaya kwa upesi.

Adhabu zimeandaliwa kwa ajili ya wenye dhihaka

na mapigo kwa ajili ya migongo ya wapumbavu.

Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu. Copyright © 2018, 2024 Biblica, Inc. Licensed under CC BY-SA 4.0. “Biblica” ni alama ya biashara iliyosajiliwa katika United States Patent and Trademark Office (ofisi ya hataza na alama za biashara Marekani) na shirika la Biblica, Inc. Source: eBible.org. Typeset from the source files; no intended changes to scripture wording. BibleKenya is not endorsed by the rights holder.

Full source notice & licence · CC BY-SA 4.0 · SourceEdition imported 2026-10-25.

BibleKenya

Reader settings

Theme
Font
Alignment
Reading width

Saved in this browser and used offline too. Press ? for keyboard shortcuts.