Skip to content
BibleKenya

Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu

Nahumu 1

Neno la unabii kuhusu Ninawi. Kitabu cha maono cha Nahumu Mwelkoshi.

Hasira ya Mwenyezi Mungu dhidi ya Ninawi

Mwenyezi Mungu ni mwenye wivu na Mungu mlipiza kisasi;

Mwenyezi Mungu hulipiza kisasi na amejaa ghadhabu.

Mwenyezi Mungu hulipiza kisasi juu ya watesi wake,

naye anadumisha ghadhabu yake dhidi ya adui zake.

Mwenyezi Mungu si mwepesi wa hasira naye ni mwenye nguvu,

Mwenyezi Mungu hataacha kuadhibu wenye hatia.

Njia yake ipo katika kisulisuli na tufani,

na mawingu ni vumbi la miguu yake.

Anakemea bahari na kuikausha,

anafanya mito yote kukauka.

Bashani na Karmeli zinanyauka

na maua ya Lebanoni hukauka.

Milima hutikisika mbele yake

na vilima huyeyuka.

Nchi hutetemeka mbele yake,

dunia na wote wanaoishi ndani yake.

Ni nani awezaye kuzuia hasira yake yenye uchungu?

Nani awezaye kuvumilia hasira yake kali?

Ghadhabu yake imemiminwa kama moto,

na miamba inapasuka mbele zake.

Mwenyezi Mungu ni Mwema,

kimbilio wakati wa taabu.

Huwatunza wale wanaomtegemea,

lakini kwa mafuriko makubwa,

ataangamiza Ninawi;

atafuatilia adui zake hadi gizani.

Kila njama wanayopanga dhidi ya Mwenyezi Mungu

yeye atalikomesha;

taabu haitatokea mara ya pili.

Watasongwa katikati ya miiba

na kulewa kwa mvinyo wao.

Watateketezwa kama mabua makavu.

Ee Ninawi, kutoka kwako amejitokeza mmoja,

ambaye anapanga njama

dhidi ya Mwenyezi Mungu

na kushauri uovu.

Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu:

“Ingawa wana muungano nao ni wengi sana,

watakatiliwa mbali na kuangamia.

Ingawa nimekutesa wewe, ee Yuda,

sitakutesa tena.

Sasa nitavunja nira zao kutoka shingo yako,

nami nitazivunjilia mbali pingu zako.”

Hii ndiyo amri Mwenyezi Mungu aliyoitoa kukuhusu wewe, Ninawi:

“Hutakuwa na wazao

watakaoendeleza jina lako.

Nitaharibu sanamu za kuchonga na sanamu za kusubu

zilizopo katika hekalu la miungu yenu.

Nitaandaa kaburi lako,

kwa maana wewe ni mwovu kabisa.”

Tazama, huko juu milimani,

miguu ya huyo mmoja aletaye habari njema,

ambaye anatangaza amani!

Ee Yuda, sherehekea sikukuu zako,

nawe utimize nadhiri zako.

Waovu hawatakuvamia tena;

wataangamizwa kabisa.

Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu. Copyright © 2018, 2024 Biblica, Inc. Licensed under CC BY-SA 4.0. “Biblica” ni alama ya biashara iliyosajiliwa katika United States Patent and Trademark Office (ofisi ya hataza na alama za biashara Marekani) na shirika la Biblica, Inc. Source: eBible.org. Typeset from the source files; no intended changes to scripture wording. BibleKenya is not endorsed by the rights holder.

Full source notice & licence · CC BY-SA 4.0 · SourceEdition imported 2026-10-25.

BibleKenya

Reader settings

Theme
Font
Alignment
Reading width

Saved in this browser and used offline too. Press ? for keyboard shortcuts.