Skip to content
BibleKenya

Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu

Mika 7

Taabu ya Israeli

Taabu gani hii niliyo nayo!

Nimefanana na yule akusanyaye

matunda ya kiangazi,

aokotaye masazo baada ya kuvunwa

shamba la mizabibu;

hakuna kishada chenye matunda ya kula,

hakuna hata ile tini ya mwanzoni ninayoitamani.

Wanaomcha Mungu wameondolewa kutoka nchi;

hakuna mtu mnyofu hata mmoja aliyebaki.

Watu wote wanavizia kumwaga damu,

kila mmoja anamwinda ndugu yake kwa wavu.

Mikono yote miwili ni hodari katika kufanya ubaya,

mtawala anadai zawadi,

hakimu anapokea rushwa,

wenye nguvu wanaamuru wanachotaka:

wote wanapanga njama pamoja.

Aliye mwema kupita wote kati yao

ni kama mchongoma,

anayeonekana mnyofu zaidi miongoni mwao

ni mbaya kuliko uzio wa miiba.

Siku ya walinzi wako imewadia,

siku Mungu atakayokutembelea.

Sasa ni wakati wao

wa kuchanganyikiwa.

Usimtumaini jirani;

usiweke matumaini kwa rafiki.

Hata kwa yule alalaye kifuani mwako

uwe mwangalifu kwa maneno yako.

Kwa kuwa mwana humdharau baba yake,

naye binti huinuka dhidi ya mama yake,

mkwe kuwa kinyume na mama mkwe wake:

adui wa mtu ni wale wa nyumbani mwake hasa.

Lakini mimi, namtazama Mwenyezi Mungu kwa matumaini,

namngoja Mungu Mwokozi wangu;

Mungu wangu atanisikia mimi.

Israeli atainuka

Usifurahie msiba wangu, ee adui yangu!

Ingawa nimeanguka, nitainuka.

Japo ninaketi gizani,

Mwenyezi Mungu atakuwa nuru yangu.

Kwa sababu nimetenda dhambi dhidi yake,

nitabeba ghadhabu ya Mwenyezi Mungu,

hadi atakapotetea shauri langu

na kuithibitisha haki yangu.

Atanileta nje kwenye mwanga,

nami nitaiona haki yake.

Kisha adui yangu ataliona

naye atafunikwa na aibu,

yule aliyeniambia,

“Yu wapi Mwenyezi Mungu, Mungu wako?”

Macho yangu yataona kuanguka kwake,

hata sasa atakanyagwa chini ya mguu

kama tope barabarani.

Siku ya kujenga kuta zako itawadia,

siku ya kupanua mipaka yako.

Siku hiyo watu watakuja kwako

kutoka Ashuru na miji ya Misri,

hata kutoka Misri hadi Mto Frati,

na kutoka bahari hadi bahari,

na kutoka mlima hadi mlima.

Dunia itakuwa ukiwa kwa sababu ya wakazi wake,

kwa sababu ya matunda ya matendo yao.

Sala na sifa

Wachunge watu wako kwa fimbo yako,

kundi la urithi wako,

ambalo linaishi peke yake msituni,

katika maeneo ya malisho yenye rutuba.

Waache walishe katika Bashani na Gileadi

kama ilivyokuwa siku za kale.

“Kama siku zile mlipotoka Misri,

nitawaonesha maajabu yangu.”

Mataifa yataona na kuaibika,

waliondolewa nguvu zao zote.

Wataweka mikono yao kwenye vinywa vyao

na masikio yao yatakuwa na uziwi.

Wataramba mavumbi kama nyoka,

kama viumbe vinavyotambaa ardhini.

Watatoka nje ya mapango yao wakitetemeka;

watamgeukia Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, kwa hofu

nao watakuogopa.

Ni nani Mungu kama wewe,

ambaye anaachilia dhambi

na kusamehe makosa

ya mabaki ya urithi wake?

Wewe huwi na hasira milele,

bali unafurahia kuonesha rehema.

Utatuhurumia tena,

utazikanyaga dhambi zetu

chini ya nyayo zako,

na kutupa maovu yetu yote

katika vilindi vya bahari.

Utakuwa wa kweli kwa Yakobo,

nawe utamwonesha Ibrahimu rehema,

kama ulivyowaahidi kwa kiapo baba zetu

siku za kale.

Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu. Copyright © 2018, 2024 Biblica, Inc. Licensed under CC BY-SA 4.0. “Biblica” ni alama ya biashara iliyosajiliwa katika United States Patent and Trademark Office (ofisi ya hataza na alama za biashara Marekani) na shirika la Biblica, Inc. Source: eBible.org. Typeset from the source files; no intended changes to scripture wording. BibleKenya is not endorsed by the rights holder.

Full source notice & licence · CC BY-SA 4.0 · SourceEdition imported 2026-10-25.

BibleKenya

Reader settings

Theme
Font
Alignment
Reading width

Saved in this browser and used offline too. Press ? for keyboard shortcuts.