Skip to content
BibleKenya

Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu

Ayubu 11

Sofari anasema: Hatia ya Ayubu inastahili adhabu

Ndipo Sofari Mnaamathi akajibu:

“Je, maneno haya yote yapite bila kujibiwa?

Je, huyu mnenaji athibitishwe kuwa na haki?

Je, maneno yako ya upuzi yawafanye watu wanyamaze kimya?

Je, mtu asikukemee unapofanya dhihaka?

Unamwambia Mungu, ‘Imani yangu ni kamili

nami ni safi mbele zako.’

Aha! Laiti kwamba Mungu angesema,

kwamba angefungua midomo yake dhidi yako,

naye akufunulie siri za hekima,

kwa kuwa hekima ya kweli ina pande mbili.

Ujue hili: Mungu amesahau hata baadhi ya dhambi zako.

“Je, unaweza kujua siri za Mungu?

Je, unaweza kuyachunguza mambo yote kumhusu Mwenyezi?

Ni juu mno kuliko mbingu: unaweza kufanya nini?

Kina chake ni kirefu kuliko Kuzimu1:

wewe unaweza kujua nini?

Kipimo chake ni kirefu kuliko dunia,

nacho ni kipana kuliko bahari.

“Akija na kukufunga gerezani,

na kuitisha mahakama, ni nani awezaye kumpinga?

Hakika anawatambua watu wadanganyifu;

naye aonapo uovu, je, haangalii?

Mpumbavu aweza kuwa mwenye hekima,

endapo mtoto wa punda-mwitu atazaliwa mwanadamu.

“Hata sasa ukiutoa moyo wako kwake

na kumwinulia mikono yako,

ukiiondolea mbali ile dhambi iliyo mkononi mwako,

wala usiuruhusu uovu ukae kwenye hema lako,

ndipo utainua uso wako bila aibu;

utasimama imara bila hofu.

Hakika utaisahau taabu yako,

utaikumbuka tu kama maji yaliyokwisha kupita.

Maisha yako yatang’aa kuliko adhuhuri,

nalo giza litakuwa kama alfajiri.

Utakuwa salama, kwa kuwa lipo tumaini;

utatazama pande zote na kupumzika kwa salama.

Utalala, wala hakuna atakayekuogofya,

naam, wengi watajipendekeza kwako.

Bali macho ya waovu hayataona,

wokovu utawaepuka;

tarajio lao litakuwa ni hangaiko

la mtu anayekata roho.”

Source notes (1)
  1. Footnote Kuzimu kwa Kiebrania ni Sheol , yaani Shimo lisilo na mwisho.

Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu. Copyright © 2018, 2024 Biblica, Inc. Licensed under CC BY-SA 4.0. “Biblica” ni alama ya biashara iliyosajiliwa katika United States Patent and Trademark Office (ofisi ya hataza na alama za biashara Marekani) na shirika la Biblica, Inc. Source: eBible.org. Typeset from the source files; no intended changes to scripture wording. BibleKenya is not endorsed by the rights holder.

Full source notice & licence · CC BY-SA 4.0 · SourceEdition imported 2026-10-25.

BibleKenya

Reader settings

Theme
Font
Alignment
Reading width

Saved in this browser and used offline too. Press ? for keyboard shortcuts.