Skip to content
BibleKenya

Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu

Ayubu 10

Ayubu anaendelea

“Nayachukia sana haya maisha yangu;

kwa hiyo nitatoa malalamiko yangu kwa wazi bila kujizuia,

nami nitanena kutokana na uchungu wa moyo wangu.

Nitamwambia Mungu: Usinihukumu,

bali niambie una mashtaka gani dhidi yangu.

Je, inakupendeza wewe kunidhulumu,

kuikataa kazi ya mikono yako,

huku ukiunga mkono mipango ya waovu?

Je, wewe una macho ya kimwili?

Je, wewe huona kama mwanadamu aonavyo?

Je, siku zako ni kama zile za mwanadamu,

au miaka yako ni kama ile ya mtu,

ili utafute makosa yangu

na kuichunguza dhambi yangu;

ingawa unajua kuwa mimi sina hatia,

na hakuna awezaye kunitoa mkononi mwako?

“Mikono yako ndiyo iliyoniumba na kunifanya.

Je, sasa utageuka na kuniangamiza?

Kumbuka kuwa ulinifinyanga kama udongo wa mfinyanzi.

Je, sasa utanifanya kuwa mavumbi tena?

Je, wewe hukunimimina mimi kama maziwa,

na kunigandisha kama jibini,

ukanivika ngozi na nyama,

na kuniunga pamoja kwa mifupa na mishipa?

Umenipa uhai na kunitendea wema,

katika uangalizi wako umeilinda roho yangu.

“Lakini hili ndilo ulilolificha moyoni mwako,

nami ninajua kuwa hili lilikuwa katika nia yako:

Kama nilifanya dhambi, ungekuwa umeniona,

wala usingeacha kosa langu lipite bila kuadhibiwa.

Kama nina hatia, ole wangu!

Hata kama ningekuwa sina hatia,

siwezi kukiinua kichwa changu,

kwa kuwa nimejawa na aibu,

na kuzama katika mateso yangu.

Nikiinua kichwa changu juu, unaniwinda kama simba,

na kuonesha tena uwezo wa kutisha dhidi yangu.

Wewe waleta mashahidi wapya dhidi yangu

na kuzidisha hasira yako juu yangu;

nazo nguvu zako zinanijia wimbi moja baada ya jingine.

“Kwa nini basi ulinitoa tumboni?

Ninatamani ningekufa kabla jicho lolote halijaniona.

Laiti nisingezaliwa,

au kama ningepelekwa kaburini

moja kwa moja kutoka tumboni!

Je, siku zangu chache si zimekaribia kwisha?

Niachie ili niweze kupata muda mfupi wa kufurahi

kabla sijaenda mahali ambapo hakuna kurudi tena,

katika nchi ya giza na uvuli wa mauti,

nchi ya giza nene sana,

yenye uvuli wa giza na machafuko,

ambapo hata nuru ni giza.”

Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu. Copyright © 2018, 2024 Biblica, Inc. Licensed under CC BY-SA 4.0. “Biblica” ni alama ya biashara iliyosajiliwa katika United States Patent and Trademark Office (ofisi ya hataza na alama za biashara Marekani) na shirika la Biblica, Inc. Source: eBible.org. Typeset from the source files; no intended changes to scripture wording. BibleKenya is not endorsed by the rights holder.

Full source notice & licence · CC BY-SA 4.0 · SourceEdition imported 2026-10-25.

BibleKenya

Reader settings

Theme
Font
Alignment
Reading width

Saved in this browser and used offline too. Press ? for keyboard shortcuts.