Skip to content
BibleKenya

Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu

Hosea 11

Upendo wa Mwenyezi Mungu kwa Israeli

“Israeli alipokuwa mtoto, nilimpenda;

nilimwita mwanangu kutoka Misri.

Lakini kadiri nilivyomwita Israeli,

ndivyo walivyoenda mbali nami.

Walitoa dhabihu kwa Mabaali

na kufukiza uvumba kwa vinyago.

Mimi ndiye niliyemfundisha Efraimu kutembea,

nikiwashika mikono;

lakini hawakutambua

kuwa ni mimi niliyewaponya.

Niliwaongoza kwa kamba za huruma ya kibinadamu,

kwa vifungo vya upendo;

niliondoa nira shingoni mwao

nami nikainama kuwalisha.

“Je, hawatarudi Misri,

nayo Ashuru haitawatawala

kwa sababu wamekataa kutubu?

Upanga utavurumishwa katika miji yao,

nao utaharibu makomeo ya malango yao

na kukomesha mipango yao.

Watu wangu wamedhamiria kuniacha.

Hata wakimwita Yeye Aliye Juu Sana,

kwa vyovyote hatawainua.

“Efraimu, ninawezaje kukuacha?

Ee Israeli, ninawezaje kukutoa?

Nitawezaje kukutendea kama Adma?

Nitawezaje kukufanya kama Seboimu?

Moyo wangu umegeuka ndani yangu,

huruma zangu zote zimeamshwa.

Sitatimiza hasira yangu kali,

wala sitageuka na kumharibu Efraimu.

Kwa kuwa mimi ndimi Mungu,

wala si mwanadamu,

Aliye Mtakatifu miongoni mwenu.

Sitakuja kwa ghadhabu.

Watamfuata Mwenyezi Mungu;

atanguruma kama simba.

Anaponguruma,

watoto wake watakuja wakitetemeka

kutoka magharibi.

Watakuja wakitetemeka

kama ndege wakitoka Misri,

kama hua wakitoka Ashuru.

Nitawafanya waishi katika nyumba zao,”

asema Mwenyezi Mungu.

Dhambi ya Israeli

Efraimu amenizunguka kwa uongo,

nyumba ya Israeli kwa udanganyifu.

Naye Yuda ni mkaidi dhidi ya Mungu,

hata kinyume cha yule mwaminifu Aliye Mtakatifu.

Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu. Copyright © 2018, 2024 Biblica, Inc. Licensed under CC BY-SA 4.0. “Biblica” ni alama ya biashara iliyosajiliwa katika United States Patent and Trademark Office (ofisi ya hataza na alama za biashara Marekani) na shirika la Biblica, Inc. Source: eBible.org. Typeset from the source files; no intended changes to scripture wording. BibleKenya is not endorsed by the rights holder.

Full source notice & licence · CC BY-SA 4.0 · SourceEdition imported 2026-10-25.

BibleKenya

Reader settings

Theme
Font
Alignment
Reading width

Saved in this browser and used offline too. Press ? for keyboard shortcuts.