Skip to content
BibleKenya

Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu

Hosea 10

Israeli alikuwa mzabibu uliostawi sana,

alijizalia matunda mwenyewe.

Kadiri matunda yake yalivyoongezeka,

alijenga madhabahu zaidi;

kadiri nchi yake ilivyostawi,

alipamba mawe yake ya ibada.

Moyo wao ni mdanganyifu,

nao sasa lazima wachukue hatia yao.

Mwenyezi Mungu atabomoa madhabahu zao

na kuharibu mawe yao ya ibada.

Kisha watasema, “Hatuna mfalme

kwa sababu hatukumheshimu Mwenyezi Mungu.

Lakini hata kama tungekuwa na mfalme,

angeweza kutufanyia nini?”

Wanaweka ahadi nyingi,

huapa viapo vya uongo

wanapofanya mapatano;

kwa hiyo mashtaka huchipuka

kama magugu ya sumu

katika shamba lililolimwa.

Watu wanaoishi Samaria huogopa

kwa ajili ya sanamu ya ndama ya Beth-Aveni1.

Watu wake wataiombolezea,

vivyo hivyo kuhani wake wa kuabudu sanamu,

wale waliokuwa wamefurahia fahari yake,

kwa sababu itaondolewa kutoka kwao

kwenda uhamishoni.

Itachukuliwa kwenda Ashuru

kama ushuru kwa mfalme mkuu.

Efraimu atafedheheshwa;

Israeli ataaibika kwa ajili ya sanamu zake za mti.

Samaria na mfalme wake wataelea

kama kijiti juu ya maji.

Mahali pa juu pa uovu2 pataharibiwa:

ndiyo dhambi ya Israeli.

Miiba na mibaruti itaota

na kufunika madhabahu zao.

Kisha wataiambia milima, “Tufunikeni!”

na vilima, “Tuangukieni!”

“Tangu siku za Gibea, umetenda dhambi, ee Israeli,

huko ndiko ulibaki.

Je, vita havikuwapata

watenda maovu huko Gibea?

Wakati nitakapopenda, nitawaadhibu;

mataifa yatakusanywa dhidi yao

ili kuwaweka katika vifungo

kwa ajili ya dhambi zao mbili.

Efraimu ni ndama jike aliyefundishwa

ambaye hupenda kupura;

hivyo nitamfunga nira

juu ya shingo yake nzuri.

Nitamwendesha Efraimu,

Yuda lazima alime,

naye Yakobo lazima avunjavunje

mabonge ya udongo.

Jipandieni wenyewe haki,

vuneni matunda ya upendo usio na kikomo,

vunjeni ardhi yenu isiyolimwa;

kwa kuwa ni wakati wa kumtafuta Mwenyezi Mungu,

hadi atakapokuja

na kuwanyeshea juu yenu haki.

Lakini mmepanda uovu,

mkavuna ubaya,

mmekula tunda la udanganyifu.

Kwa sababu mmetegemea nguvu zenu wenyewe

na wingi wa mashujaa wenu,

mngurumo wa vita utainuka dhidi ya watu wako,

na ngome zako zote zitaharibiwa:

kama Shalmani alivyoharibu Beth-Arbeli katika siku ile ya vita,

wakati mama pamoja na watoto wao

walipotupwa kwa nguvu ardhini.

Ndivyo itakavyotokea kwako, ee Betheli,

kwa sababu uovu wako ni mkuu.

Siku ile itakapopambazuka,

mfalme wa Israeli ataharibiwa kabisa.

Source notes (2)
  1. Footnote maana yake Nyumba ya Ubatili (au Uovu ); yaani Betheli kwa dhihaka
  2. Footnote yaani Aveni kwa Kiebrania, kumaanisha Beth-Aveni

Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu. Copyright © 2018, 2024 Biblica, Inc. Licensed under CC BY-SA 4.0. “Biblica” ni alama ya biashara iliyosajiliwa katika United States Patent and Trademark Office (ofisi ya hataza na alama za biashara Marekani) na shirika la Biblica, Inc. Source: eBible.org. Typeset from the source files; no intended changes to scripture wording. BibleKenya is not endorsed by the rights holder.

Full source notice & licence · CC BY-SA 4.0 · SourceEdition imported 2026-10-25.

BibleKenya

Reader settings

Theme
Font
Alignment
Reading width

Saved in this browser and used offline too. Press ? for keyboard shortcuts.