Skip to content
BibleKenya

Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu

Kumbukumbu 16

Pasaka

(Kutoka 12:1-20)

Shikeni mwezi wa Abibu, na kuiadhimisha Pasaka ya Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, kwa sababu katika mwezi wa Abibu, Mungu aliwatoa Misri usiku. Mtatoa dhabihu ya Pasaka ya mnyama kwa Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, kutoka kundi lenu la mbuzi na kondoo, au la ng’ombe, mahali atakapopachagua Mwenyezi Mungu kuwa makao kwa ajili ya Jina lake. Msile nyama hiyo pamoja na mikate iliyotiwa chachu, lakini kwa siku saba mtakula mikate isiyotiwa chachu, mikate ya kujitesa, kwa sababu mliondoka Misri kwa haraka, ili siku zote za maisha yenu mpate kukumbuka wakati wenu wa kuondoka Misri. Chachu isionekane kwenu katika nchi yenu yote kwa siku saba. Nyama yoyote ya dhabihu mtakayotoa jioni ya siku ya kwanza isibakizwe hadi asubuhi.

Kamwe msitoe dhabihu ya Pasaka katika mji wowote ambao Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, amewapa, isipokuwa mahali atakapopachagua kuwa makao kwa ajili ya Jina lake. Hapo lazima mtoe dhabihu ya Pasaka jioni jua litakapotua, iwe kumbukumbu yenu ya kutoka Misri. Okeni na mle mahali atakapopachagua Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, kisha asubuhi mrudi kwenye mahema yenu. Kwa siku sita mtakula mikate isiyotiwa chachu na siku ya saba fanyeni kusanyiko kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, na msifanye kazi.

Sikukuu ya Mavuno

(Kutoka 34:22; Walawi 23:15-21)

Mhesabu majuma saba tangu wakati mnapoanza kuchukua mundu kuvuna nafaka. Kisha msherehekee Sikukuu ya Majuma kwa Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, kwa kutoa sadaka ya hiari kwa kadiri ya baraka ambayo Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, amewapa. Shangilieni mbele za Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, mahali atakapopachagua kuwa makao ya Jina lake, ninyi, wana wenu na binti zenu, watumishi wenu wa kiume na wa kike, Walawi walio katika miji yenu, na wageni, yatima na wajane wanaoishi miongoni mwenu. Kumbukeni kwamba mlikuwa watumwa kule Misri na mfuate amri hizi kwa uangalifu.

Sikukuu ya Vibanda

(Walawi 23:33-43)

Adhimisheni sikukuu ya vibanda kwa siku saba baada ya kukusanya mazao kutoka sakafu yako ya kupuria nafaka, na kutoka shinikizo lako la kukamulia zabibu. Mfurahie sikukuu yenu, ninyi, wana wenu, binti zenu, watumishi wenu wa kiume na wa kike, Walawi, wageni, yatima na wajane ambao wanaishi katika miji yenu. Kwa siku saba mtaiadhimisha sikukuu ya Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, katika mahali atakapopachagua Mwenyezi Mungu. Kwa kuwa Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, atawabariki katika mavuno yenu na katika kazi zote za mikono yenu na furaha yenu itakamilika.

Wanaume wenu wote lazima wajitokeze mara tatu kwa mwaka mbele za Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, mahali atakapopachagua: kwa ajili ya Sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu, Sikukuu ya Majuma, na Sikukuu ya Vibanda. Hakuna mtu atakayejitokeza mbele za Mwenyezi Mungu mikono mitupu: Kila mmoja wenu ni lazima alete zawadi kulingana na jinsi Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, alivyowabariki.

Waamuzi

Wateue waamuzi na maafisa kwa kila kabila lenu katika kila mji ambao Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, anawapa, nao watawaamua watu kwa usawa. Msipotoshe haki wala msifanye upendeleo. Msikubali rushwa kwa sababu rushwa hupofusha macho ya wenye busara na kugeuza maneno ya wenye haki. Mfuate haki na haki peke yake, ili mweze kuishi na kuimiliki nchi ambayo Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, anawapa.

Kuabudu miungu mingine

Msisimamishe nguzo yoyote ya Ashera kando ya madhabahu mliyomjengea Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, wala msisimamishe jiwe la kuabudu, kwa maana Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, anavichukia vitu hivi.

Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu. Copyright © 2018, 2024 Biblica, Inc. Licensed under CC BY-SA 4.0. “Biblica” ni alama ya biashara iliyosajiliwa katika United States Patent and Trademark Office (ofisi ya hataza na alama za biashara Marekani) na shirika la Biblica, Inc. Source: eBible.org. Typeset from the source files; no intended changes to scripture wording. BibleKenya is not endorsed by the rights holder.

Full source notice & licence · CC BY-SA 4.0 · SourceEdition imported 2026-10-25.

BibleKenya

Reader settings

Theme
Font
Alignment
Reading width

Saved in this browser and used offline too. Press ? for keyboard shortcuts.