Skip to content
BibleKenya

Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu

2 Wakorintho 9

Wasaidieni wafuasi wa Al-Masihi wenzenu

Hakuna haja ya kuwaandikia kuhusu huduma hii kwa watakatifu. Kwa kuwa ninajua mlivyo na shauku ya kusaidia, nami nimekuwa nikijivuna kwa ajili ya jambo hilo kwa Wamakedonia, nikiwaambia kwamba ninyi watu wa Akaya mmekuwa tayari kutoa tangu mwaka jana. Na shauku yenu imewachochea wengi wao katika kutoa. Lakini sasa nawatuma hawa ndugu ili kujivuna kwetu kuhusu mchango wenu kusiwe maneno matupu, bali mpate kuwa tayari kama nilivyosema mngekuwa tayari. Kwa maana nikija na Mmakedonia yeyote na kuwakuta hamko tayari, sisi, na hata ninyi pia, tungeona haya kwa kuwa na ujasiri hivi katika ninyi. Kwa hivyo niliona ni muhimu niwahimize hawa ndugu watangulie kuja huko kwenu kabla yangu, wafanye mipango ya hayo matoleo ya ukarimu mliyokuwa mmeahidi, ili yawe tayari kama matoleo ya hiari wala si kama ya kutozwa kwa nguvu.

Kupanda kwa ukarimu

Kumbukeni kwamba: Yeyote apandaye haba pia atavuna haba, naye apandaye kwa ukarimu pia atavuna kwa ukarimu. Kila mtu atoe kama anavyokusudia moyoni mwake, si kwa uchoyo au kwa kulazimishwa, kwa maana Mungu humpenda yeye atoaye kwa moyo mkunjufu. Naye Mungu aweza kuwapa kila baraka kwa wingi, ili katika mambo yote kila wakati mwe na kila kitu mnachohitaji, ili mweze kushiriki kwa wingi katika kila kazi njema. Kama ilivyoandikwa:

“Ametawanya vipawa vyake kwa ukarimu akawapa maskini;

haki yake hudumu milele.”

Yeye ampaye mpanzi mbegu ya kupanda, na mkate uwe chakula, atawapa na kuzizidisha mbegu zenu za kupanda na kuongeza mavuno ya haki yenu. Mtatajirishwa kwa kila namna ili mpate kuwa wakarimu kila wakati, na kupitia kwetu ukarimu wenu utamletea Mungu shukrani.

Huduma hii mnayofanya si tu ya kukidhi mahitaji ya watakatifu, bali huzidi sana kwa shukrani nyingi kwake Mungu. Kwa sababu ya huduma ambayo mmejithibitisha wenyewe, watu watamtukuza Mungu kwa ajili ya utiifu ufuatanao na ukiri wenu wa Injili ya Al-Masihi, na kwa ukarimu wenu wa kuwashirikisha wao na watu wengine wote. Nayo mioyo yao itawaonea shauku wanapowaombea, kwa sababu ya neema ipitayo kiasi mliyopewa na Mungu. Mungu apewe shukrani kwa karama yake isiyoelezeka!

Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu. Copyright © 2018, 2024 Biblica, Inc. Licensed under CC BY-SA 4.0. “Biblica” ni alama ya biashara iliyosajiliwa katika United States Patent and Trademark Office (ofisi ya hataza na alama za biashara Marekani) na shirika la Biblica, Inc. Source: eBible.org. Typeset from the source files; no intended changes to scripture wording. BibleKenya is not endorsed by the rights holder.

Full source notice & licence · CC BY-SA 4.0 · SourceEdition imported 2026-10-25.

BibleKenya

Reader settings

Theme
Font
Alignment
Reading width

Saved in this browser and used offline too. Press ? for keyboard shortcuts.