Skip to content
BibleKenya

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™

Zaburi 17

Sala Ya Mtu Asiye Na Hatia

Sala ya Daudi.

Sikia, Ee Bwana, kusihi kwangu kwa haki,

sikiliza kilio changu.

Tega sikio kwa ombi langu,

halitoki kwenye midomo ya udanganyifu.

Hukumu yangu na itoke kwako,

macho yako na yaone yale yaliyo haki.

Ingawa unauchunguza moyo wangu na kunikagua usiku,

ingawa umenijaribu, hutaona chochote.

Nimeamua kwamba kinywa changu

hakitatenda dhambi.

Kuhusu matendo ya wanadamu:

kwa neno la midomo yako,

nimejiepusha

na njia za wenye jeuri.

Hatua zangu zimeshikamana na njia zako;

nyayo zangu hazikuteleza.

Ee Mungu, ninakuita, kwa kuwa utanijibu,

nitegee sikio lako na usikie ombi langu.

Uonyeshe ajabu ya upendo wako mkuu,

wewe uokoaye kwa mkono wako wa kuume

wale wanaokukimbilia kutokana na adui zao.

Nilinde kama mboni ya jicho lako,

unifiche chini ya kivuli cha mbawa zako

kutokana na waovu wanaonishambulia,

kutokana na adui wauaji wanaonizunguka.

Huifunga mioyo yao iliyo migumu,

vinywa vyao hunena kwa majivuno.

Wamenifuatia nyayo zangu, sasa wamenizingira,

wakiwa macho, waniangushe chini.

Wamefanana na simba mwenye njaa awindaye,

kama simba mkubwa anyemeleaye mafichoni.

Inuka, Ee Bwana, pambana nao, uwaangushe,

niokoe kutokana na waovu kwa upanga wako.

Ee Bwana, mkono wako uniokoe na watu wa jinsi hii,

kutokana na watu wa ulimwengu huu

ambao fungu lao liko katika maisha haya.

Na wapate adhabu ya kuwatosha.

Watoto wao na wapate zaidi ya hayo,

hukumu na iendelee kwa watoto wa watoto wao.

Na mimi katika haki nitauona uso wako,

niamkapo, nitaridhika kwa kuona sura yako.

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™. Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015 Biblica, Inc. Licensed under CC BY-SA 4.0. Source: eBible.org. Typeset from the source files; no intended changes to scripture wording. BibleKenya is not endorsed by the rights holder.

Full source notice & licence · CC BY-SA 4.0 · SourceEdition imported 2026-10-25.

BibleKenya

Reader settings

Theme
Font
Alignment
Reading width

Saved in this browser and used offline too. Press ? for keyboard shortcuts.