Skip to content
BibleKenya

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™

Zaburi 16

Sala Ya Matumaini

Utenzi wa Daudi.

Ee Mungu, uniweke salama,

kwa maana kwako nimekimbilia.

Nilimwambia Bwana, “Wewe ndiwe Bwana wangu;

pasipo wewe sina jambo jema.”

Kwa habari ya watakatifu walioko duniani,

ndio walio wa fahari ambao ninapendezwa nao.

Huzuni itaongezeka kwa wale

wanaokimbilia miungu mingine.

Sitazimimina sadaka zao za damu

au kutaja majina yao midomoni mwangu.

Bwana umeniwekea fungu langu na kikombe changu;

umeyafanya mambo yangu yote yawe salama.

Alama za mipaka zimeniangukia mahali pazuri,

hakika nimepata urithi mzuri.

Nitamsifu Bwana ambaye hunishauri,

hata wakati wa usiku moyo wangu hunifundisha.

Nimemweka Bwana mbele yangu daima.

Kwa sababu yuko mkono wangu wa kuume,

sitatikisika.

Kwa hiyo moyo wangu unafurahia, na ulimi wangu unashangilia;

mwili wangu nao utapumzika salama,

kwa maana hutaniacha kaburini,

wala hutamwacha Mtakatifu Wako kuona uharibifu.

Umenijulisha njia ya uzima;

utanijaza na furaha mbele zako,

pamoja na furaha za milele

katika mkono wako wa kuume.

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™. Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015 Biblica, Inc. Licensed under CC BY-SA 4.0. Source: eBible.org. Typeset from the source files; no intended changes to scripture wording. BibleKenya is not endorsed by the rights holder.

Full source notice & licence · CC BY-SA 4.0 · SourceEdition imported 2026-10-25.

BibleKenya

Reader settings

Theme
Font
Alignment
Reading width

Saved in this browser and used offline too. Press ? for keyboard shortcuts.