Skip to content
BibleKenya

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™

Zaburi 141

Maombi Ya Kuhifadhiwa Dhidi Ya Uovu

Zaburi ya Daudi.

Ee Bwana, ninakuita wewe, uje kwangu hima.

Sikia sauti yangu ninapokuita.

Maombi yangu na yafike mbele zako kama uvumba;

kuinua mikono yangu juu na kuwe kama dhabihu ya jioni.

Ee Bwana, weka mlinzi kinywani mwangu,

weka ulinzi mlangoni mwa midomo yangu.

Usiuache moyo wangu uvutwe katika jambo baya,

nisije nikashiriki katika matendo maovu

pamoja na watu watendao mabaya,

wala nisije nikala vyakula vyao vya anasa.

Mtu mwenye haki na anipige: ni jambo la huruma;

na anikemee: ni mafuta kichwani mwangu.

Kichwa changu hakitalikataa.

Hata hivyo, maombi yangu daima

ni kinyume cha watenda mabaya,

watawala wao watatupwa chini

kutoka kwenye majabali,

waovu watajifunza kwamba maneno yangu

yalikuwa kweli.

Watasema, “Kama mtu anavyolima na kuvunja ardhi,

ndivyo mifupa yetu imetawanywa kwenye mlango wa kaburi.”

Lakini nimekaza macho yangu kwako, Ee Bwana Mwenyezi,

ndani yako nimekimbilia, usiniache nife.

Niepushe na mitego waliyonitegea,

kutokana na mitego iliyotegwa na watenda mabaya.

Waovu na waanguke kwenye nyavu zao wenyewe,

wakati mimi ninapita salama.

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™. Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015 Biblica, Inc. Licensed under CC BY-SA 4.0. Source: eBible.org. Typeset from the source files; no intended changes to scripture wording. BibleKenya is not endorsed by the rights holder.

Full source notice & licence · CC BY-SA 4.0 · SourceEdition imported 2026-10-25.

BibleKenya

Reader settings

Theme
Font
Alignment
Reading width

Saved in this browser and used offline too. Press ? for keyboard shortcuts.