Skip to content
BibleKenya

Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu

Sefania 2

Hukumu dhidi ya mataifa

Dhidi ya Yuda

Kusanyikeni pamoja, kusanyikeni pamoja,

enyi taifa lisilo na aibu,

kabla wakati ulioamriwa haujafika

na siku ile inayopeperusha kama makapi,

kabla hasira kali ya Mwenyezi Mungu haijaja juu yenu,

kabla siku ya ghadhabu ya Mwenyezi Mungu

haijaja juu yenu.

Mtafuteni Mwenyezi Mungu, enyi nyote wanyenyekevu wa nchi,

ninyi ambao hufanya lile analoamuru.

Tafuteni haki, tafuteni unyenyekevu;

labda mtahifadhiwa

siku ya hasira ya Mwenyezi Mungu.

Dhidi ya Ufilisti

Gaza utaachwa

na Ashkeloni utaachwa magofu.

Wakati wa adhuhuri Ashdodi utaachwa mtupu,

na Ekroni utang’olewa.

Ole wenu ninyi ambao mnaishi kando ya bahari,

enyi Wakerethi;

neno la Mwenyezi Mungu liko dhidi yenu,

ee Kanaani, nchi ya Wafilisti.

“Mimi nitawaangamiza,

na hakuna atakayebaki.”

Nchi iliyo karibu na bahari itakuwa malisho

yenye visima vya wachungaji,

na mazizi ya kondoo.

Itakuwa mali ya mabaki ya nyumba ya Yuda,

hapo watapata malisho.

Wakati wa jioni watajilaza chini

katika nyumba za Ashkeloni.

Mwenyezi Mungu, Mungu wao, atawatunza,

naye atawarudishia wafungwa wao.

Dhidi ya Moabu na Amoni

“Nimeyasikia matukano ya Moabu

nazo dhihaka za Waamoni,

ambao waliwatukana watu wangu

na kutoa vitisho dhidi ya nchi yao.

Hakika, kama niishivyo,”

asema Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni,

Mungu wa Israeli,

“hakika Moabu itakuwa kama Sodoma,

Waamoni kama Gomora:

mahali pa magugu na mashimo ya chumvi,

nchi ya ukiwa milele.

Mabaki ya watu wangu watawateka nyara;

mabaki ya taifa langu watarithi nchi yao.”

Hiki ndicho watarudishiwa kwa ajili ya kiburi chao,

kwa kutukana na kudhihaki

watu wa Mwenyezi Mungu,

Mungu wa majeshi ya mbinguni.

Mwenyezi Mungu atakuwa wa kuhofisha kwao

atakapoangamiza miungu yote ya nchi.

Mataifa katika kila pwani yatamwabudu,

kila moja katika nchi yake.

Dhidi ya Kushi

“Ninyi pia, ee Wakushi,

mtauawa kwa upanga wangu.”

Dhidi ya Ashuru

Mungu atanyoosha mkono wake dhidi ya kaskazini

na kuangamiza Waashuru,

akiiacha Ninawi ukiwa

na pakame kama jangwa.

Makundi ya kondoo na ng’ombe yatajilaza pale,

viumbe vya kila aina.

Bundi wa jangwani na bundi waliao kwa sauti nyembamba

wataishi juu ya nguzo zake.

Mwangwi wa kuita kwao utapita madirishani,

kifusi kitakuwa milangoni,

boriti za mwerezi zitaachwa wazi.

Huu ndio mji uliotukuka na kuishi kwa furaha

wakijisikia salama.

Ulisema moyoni mwako,

“Mimi ndimi, na wala hapana mwingine ila mimi.”

Jinsi gani umekuwa gofu,

mahali pa kulala wanyama pori!

Wote wanaopita kando yake wanauzomea

na kutikisa mkono kwa dharau.

Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu. Copyright © 2018, 2024 Biblica, Inc. Licensed under CC BY-SA 4.0. “Biblica” ni alama ya biashara iliyosajiliwa katika United States Patent and Trademark Office (ofisi ya hataza na alama za biashara Marekani) na shirika la Biblica, Inc. Source: eBible.org. Typeset from the source files; no intended changes to scripture wording. BibleKenya is not endorsed by the rights holder.

Full source notice & licence · CC BY-SA 4.0 · SourceEdition imported 2026-10-25.

BibleKenya

Reader settings

Theme
Font
Alignment
Reading width

Saved in this browser and used offline too. Press ? for keyboard shortcuts.