Skip to content
BibleKenya

Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu

Zekaria 9

Hukumu juu ya adui za Israeli

Neno la unabii:

Neno la Mwenyezi Mungu liko kinyume na nchi ya Hadraki

na Dameski itakuwa mahali pa kupumzika,

kwa kuwa macho ya watu na ya makabila yote ya Israeli

yako kwa Mwenyezi Mungu;

pia juu ya Hamathi inayopakana nayo,

juu ya Tiro na Sidoni,

ingawa wana ujuzi mwingi sana.

Tiro amejijengea ngome imara,

amelundika fedha kama mavumbi,

na dhahabu kama taka za mitaani.

Lakini Bwana atamwondolea mali yake

na kuuangamiza uwezo wake wa baharini,

naye atateketezwa kwa moto.

Ashkeloni ataona hili na kuogopa;

Gaza atagaagaa kwa maumivu makali,

pia Ekroni, kwa sababu

matumaini yake yatanyauka.

Gaza atampoteza mfalme wake

na Ashkeloni ataachwa pweke.

Wageni watakalia mji wa Ashdodi,

nami nitakatilia mbali kiburi cha Wafilisti.

Nitaondoa damu vinywani mwao,

chakula kile walichokatazwa kati ya meno yao.

Mabaki yao yatakuwa mali ya Mungu wetu,

nao watakuwa viongozi katika Yuda,

naye Ekroni atakuwa kama Wayebusi.

Lakini nitailinda nyumba yangu

dhidi ya majeshi ya wanyang’anyi.

Kamwe mdhalimu hatashambulia watu wangu tena,

kwa maana sasa ninawachunga.

Kuja kwa Mfalme wa Sayuni

Shangilia sana, ee Binti Sayuni!

Piga kelele, Binti Yerusalemu!

Tazama, Mfalme wako anakuja kwako,

ni mwenye haki, naye ana wokovu,

ni mpole, naye amepanda punda,

mwana-punda, mtoto wa punda.

Nitaondoa magari ya vita kutoka Efraimu

na farasi wa vita kutoka Yerusalemu,

nao upinde wa vita utavunjwa.

Atatangaza amani kwa mataifa.

Utawala wake utaenea kutoka bahari hadi bahari,

na kutoka Mto1 hadi mwisho wa dunia.

Kwako wewe, kwa sababu ya damu ya agano langu nawe,

nitawaacha huru wafungwa wako

watoke kwenye shimo lisilo na maji.

Rudieni ngome yenu, enyi wafungwa wa tumaini;

hata sasa ninatangaza kwamba

nitawarejesheeni maradufu.

Nitampinda Yuda kama nipindavyo upinde wangu,

nitamfanya Efraimu mshale wangu.

Nitawainua wana wako, ee Sayuni,

dhidi ya wana wako, ee Uyunani,

na kukufanya kama upanga wa shujaa wa vita.

Mwenyezi Mungu atatokea

Kisha Mwenyezi Mungu atawatokea;

mshale wake utamulika kama radi.

Bwana Mungu Mwenyezi atapiga tarumbeta,

naye atatembea katika tufani za kusini,

na Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni atawalinda.

Wataangamiza na kushinda

kwa mawe ya kutupa kwa kombeo.

Watakunywa na kunguruma kama waliolewa mvinyo;

watajaa kama bakuli linalotumika kunyunyizia

kwenye pembe za madhabahu.

Mwenyezi Mungu, Mungu wao, atawaokoa siku hiyo

kama kundi la watu wake.

Watang’ara katika nchi yake

kama vito vya thamani kwenye taji.

Jinsi gani watavutia na kuwa wazuri!

Nafaka itawastawisha vijana wanaume,

nayo divai mpya vijana wanawake.

Source notes (1)
  1. Footnote yaani Mto Frati

Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu. Copyright © 2018, 2024 Biblica, Inc. Licensed under CC BY-SA 4.0. “Biblica” ni alama ya biashara iliyosajiliwa katika United States Patent and Trademark Office (ofisi ya hataza na alama za biashara Marekani) na shirika la Biblica, Inc. Source: eBible.org. Typeset from the source files; no intended changes to scripture wording. BibleKenya is not endorsed by the rights holder.

Full source notice & licence · CC BY-SA 4.0 · SourceEdition imported 2026-10-25.

BibleKenya

Reader settings

Theme
Font
Alignment
Reading width

Saved in this browser and used offline too. Press ? for keyboard shortcuts.