Skip to content
BibleKenya

Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu

Zekaria 7

Sio kufunga, bali ni haki na rehema

Katika mwaka wa nne wa utawala wa Mfalme Dario, neno la Mwenyezi Mungu lilimjia Zekaria siku ya nne ya mwezi wa tisa, mwezi wa Kisleu. Watu wa Betheli walikuwa wamemtuma Shareza na Regem-Meleki pamoja na watu wao, kumsihi Mwenyezi Mungu kwa kuwauliza makuhani wa nyumba ya Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni na manabii, “Je, imempasa kuomboleza na kufunga katika mwezi wa tano, kama ambavyo nimekuwa nikifanya kwa miaka mingi?”

Kisha neno la Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni likanijia kusema: “Waulize watu wote wa nchi na makuhani, ‘Je, mlipofunga na kuomboleza katika mwezi wa tano na wa saba kwa miaka sabini iliyopita, mlifunga kweli kwa ajili yangu? Na mlipokuwa mkila na kunywa, je, hamkuwa mnasherehekea kwa ajili ya nafsi zenu? Je, haya sio maneno ya Mwenyezi Mungu aliyosema kupitia manabii waliotangulia, wakati Yerusalemu pamoja na miji inayoizunguka ilipokuwa katika hali ya utulivu na ya mafanikio, wakati Negebu na Shefela1 zikiwa zimekaliwa na watu?’ ”

Neno la Mwenyezi Mungu likamjia tena Zekaria: “Hivi ndivyo asemavyo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni: ‘Fanyeni hukumu za haki, onesheni rehema na huruma ninyi kwa ninyi. Msimdhulumu mjane wala yatima, mgeni wala maskini. Msiwaziane mabaya mioyoni mwenu ninyi kwa ninyi.’

“Lakini wakakataa kusikiliza, wakanipa kisogo kwa ukaidi na kuziba masikio yao. Wakaifanya mioyo yao migumu kama gumegume, na hawakuisikiliza sheria au maneno ambayo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni aliyatuma kwa Roho wake Mtakatifu kupitia manabii waliotangulia. Kwa hiyo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, alikasirika sana.

“ ‘Nilipoita, hawakusikiliza; kwa hiyo walipoita, sikusikiliza,’ asema Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni. ‘Niliwatawanya kwa upepo wa kisulisuli miongoni mwa mataifa yote, mahali ambapo walikuwa wageni. Nchi ikaachwa ukiwa nyuma yao kiasi kwamba hakuna aliyeweza kuingia au kutoka. Hivi ndivyo walivyoifanya ile nchi iliyokuwa imependeza kuwa ukiwa.’ ”

Source notes (1)
  1. Footnote au upande wa magharibi chini ya vilima

Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu. Copyright © 2018, 2024 Biblica, Inc. Licensed under CC BY-SA 4.0. “Biblica” ni alama ya biashara iliyosajiliwa katika United States Patent and Trademark Office (ofisi ya hataza na alama za biashara Marekani) na shirika la Biblica, Inc. Source: eBible.org. Typeset from the source files; no intended changes to scripture wording. BibleKenya is not endorsed by the rights holder.

Full source notice & licence · CC BY-SA 4.0 · SourceEdition imported 2026-10-25.

BibleKenya

Reader settings

Theme
Font
Alignment
Reading width

Saved in this browser and used offline too. Press ? for keyboard shortcuts.