Skip to content
BibleKenya

Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu

Zekaria 5

Maono ya sita: Kitabu kinachoruka

Nikatazama tena: na hapo mbele yangu kulikuwa na kitabu kinachoruka!

Akaniuliza, “Unaona nini?”

Nikamjibu, “Naona kitabu kinachoruka, chenye urefu wa dhiraa ishirini1, na upana wa dhiraa kumi2.”

Akaniambia, “Hii ni laana inayotoka kwenda juu ya nchi yote, kwa kuwa kufuatana na yale yaliyoandikwa katika upande mmoja, kila mwizi atafukuziwa mbali, pia kufuatana na yaliyo upande wa pili, kila aapaye kwa uongo atafukuziwa mbali. Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni asema, ‘Nitaituma hiyo laana, nayo itaingia katika nyumba ya mwizi na nyumba ya huyo aapaye kwa uongo kwa Jina langu. Itabaki katika nyumba yake na kuiharibu, pamoja na mbao zake na mawe yake.’ ”

Maono ya saba: Mwanamke ndani ya kikapu

Kisha yule malaika aliyekuwa akizungumza nami akanijia na kuniambia, “Tazama juu uone ni nini kile kinachojitokeza.”

Nikamuuliza, “Ni kitu gani?”

Akanijibu, “Ni kikapu cha kupimia.” Kisha akaongeza kusema, “Huu ni uovu wa watu katika nchi nzima.”

Kisha kifuniko kilichotengenezwa kwa madini ya risasi kilichokuwa kimefunika kile kikapu, kiliinuliwa na ndani ya kile kikapu alikuwako mwanamke ameketi! Akasema, “Huu ni uovu,” tena akamsukumia ndani ya kikapu na kushindilia kifuniko juu ya mdomo wa kikapu.

Kisha nikatazama juu: na pale mbele yangu, palikuwa na wanawake wawili, wakiwa na upepo katika mabawa yao! Walikuwa na mabawa kama ya korongo, nao wakainua kile kikapu na kuruka nacho kati ya mbingu na nchi.

Nikamuuliza yule malaika aliyekuwa akizungumza nami, “Wanakipeleka wapi hicho kikapu?”

Akanijibu, “Wanakipeleka katika nchi ya Babeli na kujenga nyumba kwa ajili yake. Itakapokuwa tayari, kikapu kitawekwa pale mahali pake.”

Source notes (2)
  1. Footnote Dhiraa 20 ni sawa na mita 9.
  2. Footnote Dhiraa 10 ni sawa mita 4.5.

Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu. Copyright © 2018, 2024 Biblica, Inc. Licensed under CC BY-SA 4.0. “Biblica” ni alama ya biashara iliyosajiliwa katika United States Patent and Trademark Office (ofisi ya hataza na alama za biashara Marekani) na shirika la Biblica, Inc. Source: eBible.org. Typeset from the source files; no intended changes to scripture wording. BibleKenya is not endorsed by the rights holder.

Full source notice & licence · CC BY-SA 4.0 · SourceEdition imported 2026-10-25.

BibleKenya

Reader settings

Theme
Font
Alignment
Reading width

Saved in this browser and used offline too. Press ? for keyboard shortcuts.