Skip to content
BibleKenya

Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu

Zekaria 3

Maono ya nne: Mavazi safi kwa ajili ya kuhani mkuu

Kisha akanionesha Yoshua1, kuhani mkuu, akiwa amesimama mbele ya malaika wa Mwenyezi Mungu, naye Shetani amesimama upande wake wa kuume ili amshtaki. Mwenyezi Mungu akamwambia Shetani, “Mwenyezi Mungu akukemee Shetani! Mwenyezi Mungu, ambaye ameichagua Yerusalemu, akukemee! Je, mtu huyu siyo kijinga kinachowaka kilichonyakuliwa kwenye moto?”

Wakati huu, Yoshua alikuwa amevaa nguo chafu alipokuwa amesimama mbele ya malaika. Malaika akawaambia wale waliokuwa wamesimama mbele yake, “Mvueni hizo nguo zake chafu.”

Kisha akamwambia Yoshua, “Tazama, nimeiondoa dhambi yako, nami nitakuvika mavazi ya kitajiri.”

Kisha nikasema, “Mvike kilemba kilicho safi kichwani mwake.” Kwa hiyo wakamvika kilemba safi kichwani na kumvika yale mavazi mengine, wakati malaika wa Mwenyezi Mungu akiwa amesimama karibu.

Malaika wa Mwenyezi Mungu akamwamuru Yoshua: “Hivi ndivyo asemavyo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni: ‘Ikiwa utatembea katika njia zangu na kushika maagizo yangu, basi utaitawala nyumba yangu na kuzilinda nyua zangu, nami nitakupa nafasi miongoni mwa hawa wasimamao hapa.

“ ‘Sikiliza, ee Yoshua kuhani mkuu, pamoja na wenzako walioketi mbele yako, ambao ni watu walio ishara ya mambo yatakayokuja: Ninaenda kumleta mtumishi wangu, Tawi. Tazama, jiwe nililoliweka mbele ya Yoshua! Kuna macho saba juu ya jiwe lile moja, nami nitachora maandishi juu yake,’ asema Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, ‘nami nitaiondoa dhambi ya nchi hii kwa siku moja.

“ ‘Katika siku hiyo kila mmoja wenu atamwalika jirani yake akae chini ya mzabibu wake na mtini wake,’ asema Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni.”

Source notes (1)
  1. Footnote Kwa Kiebrania ni Yeshua , maana yake Yehova ni wokovu.

Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu. Copyright © 2018, 2024 Biblica, Inc. Licensed under CC BY-SA 4.0. “Biblica” ni alama ya biashara iliyosajiliwa katika United States Patent and Trademark Office (ofisi ya hataza na alama za biashara Marekani) na shirika la Biblica, Inc. Source: eBible.org. Typeset from the source files; no intended changes to scripture wording. BibleKenya is not endorsed by the rights holder.

Full source notice & licence · CC BY-SA 4.0 · SourceEdition imported 2026-10-25.

BibleKenya

Reader settings

Theme
Font
Alignment
Reading width

Saved in this browser and used offline too. Press ? for keyboard shortcuts.