Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu
Wimbo 8
Laiti ungekuwa kwangu kama ndugu wa kiume,
ambaye aliyanyonya matiti ya mama yangu!
Kisha, kama ningekukuta huko nje,
ningekubusu,
wala hakuna mtu yeyote angenidharau.
Ningekuongoza na kukuleta
katika nyumba ya mama yangu,
yeye ambaye amenifundisha.
Ningekupa divai iliyokolezwa unywe,
asali ya maua ya mikomamanga yangu.
Mkono wake wa kushoto uko chini ya kichwa changu,
na mkono wake wa kuume unanikumbatia.
Binti za Yerusalemu, ninawaagiza:
msichochee wala kuamsha mapenzi
hata yatakapotaka yenyewe.
Rafiki
Ni nani huyu anayekuja kutoka nyikani
akimwegemea mpenzi wake?
Mpendwa
Nilikuamsha chini ya mtofaa,
huko mama yako alipotunga mimba yako,
huko yeye alipata uchungu akakuzaa.
Nitie kama muhuri moyoni mwako,
kama muhuri kwenye mkono wako;
kwa maana upendo una nguvu kama mauti,
wivu wake ni mkatili kama Kuzimu1.
Unachoma kama mwali wa moto,
kama mwali mkubwa wa moto wa Mwenyezi Mungu hasa.
Maji mengi hayawezi kuuzimisha upendo,
mito haiwezi kuugharikisha.
Kama mtu angetoa mali yote ya nyumbani mwake
kwa ajili ya upendo,
angedharauliwa kabisa.
Rafiki
Tunaye dada mdogo,
matiti yake hayajakua bado.
Tutafanya nini kwa ajili ya dada yetu
wakati atakapokuja kuposwa?
Kama yeye ni ukuta,
tutajenga minara ya fedha juu yake.
Na kama yeye ni mlango,
tutamzungushia mbao za mwerezi.
Mpendwa
Mimi ni ukuta,
nayo matiti yangu ni kama minara.
Ndivyo ambavyo nimekuwa machoni pake
kama yule anayeleta utoshelevu.
Sulemani alikuwa na shamba la mizabibu huko Baal-Hamoni;
alikodisha shamba lake la mizabibu kwa wapangaji.
Kila mmoja angeleta kwa ajili ya matunda yake
shekeli elfu moja2 za fedha.
Lakini shamba langu la mizabibu
ambalo ni langu mwenyewe
ni langu kutoa;
hizo shekeli elfu moja ni kwa ajili yako, ee Sulemani,
na shekeli mia mbili3 ni kwa ajili
ya wale wanaotunza matunda yake.
Mpenzi
Wewe ukaaye bustanini
pamoja na rafiki mliohudhuria,
hebu nisikie sauti yako!
Mpendwa
Njoo, mpenzi wangu,
uwe kama paa
au kama ayala mchanga
juu ya milima iliyojaa manukato.
Source notes (3)
- Footnote Kuzimu kwa Kiebrania ni Sheol , yaani Shimo lisilo na mwisho.
- Footnote Shekeli 1,000 ni kama kilo 11.5.
- Footnote Shekeli 200 ni kama kilo 2.3.
Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu. Copyright © 2018, 2024 Biblica, Inc. Licensed under CC BY-SA 4.0. “Biblica” ni alama ya biashara iliyosajiliwa katika United States Patent and Trademark Office (ofisi ya hataza na alama za biashara Marekani) na shirika la Biblica, Inc. Source: eBible.org. Typeset from the source files; no intended changes to scripture wording. BibleKenya is not endorsed by the rights holder.
Full source notice & licence · CC BY-SA 4.0 · SourceEdition imported 2026-10-25.