Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu
Wimbo 6
Rafiki
Mpenzi wako ameenda wapi,
ewe mzuri kupita wanawake wote?
Mpenzi wako amegeukia njia ipi,
tupate kumtafuta pamoja nawe?
Mpendwa
Mpenzi wangu ameenda bustanini mwake,
kwenye vitalu vya vikolezo,
kujilisha bustanini
na kukusanya yungiyungi.
Mimi ni wake mpenzi wangu,
na mpenzi wangu ni wangu;
yeye hujilisha kati ya yungiyungi.
Mpenzi
Wewe ni mzuri, mpendwa wangu, kama Tirsa,
unapendeza kama Yerusalemu,
umetukuka kama jeshi lenye bendera.
Uyageuze macho yako mbali nami;
yananigharikisha.
Nywele zako ni kama kundi la mbuzi
wanaoteremka kutoka Gileadi.
Meno yako ni kama kundi la kondoo
wanaotoka kuogeshwa.
Kila mmoja ana pacha lake,
hakuna hata mmoja aliye peke yake.
Mashavu yako nyuma ya shela yako
ni kama vipande viwili vya komamanga.
Panaweza kuwa na malkia sitini,
masuria themanini,
na mabikira wasiohesabika;
lakini hua wangu, mkamilifu wangu,
ni wa namna ya pekee,
binti pekee kwa mama yake,
kipenzi cha yeye aliyemzaa.
Wanawali walimwona na kumwita aliyebarikiwa;
malkia na masuria walimsifu.
Rafiki
Ni nani huyu atokeaye kama mapambazuko,
mzuri kama mwezi, mwangavu kama jua,
ametukuka kama nyota zinazofuatana?
Mpenzi
Niliteremka kwenye bustani ya miti ya milozi
ili kutazama machipuko ya bondeni,
kuona kama mizabibu imechipua
au kama mikomamanga imechanua maua.
Kabla sijang’amua,
shauku yangu iliniweka
katikati ya magari ya vita ya wakuu wangu.
Rafiki
Rudi, rudi, ee Mshulami;
rudi, rudi ili tupate kukutazama!
Mpenzi
Kwa nini kumtazama Mshulami,
kama kutazama ngoma ya Mahanaimu1?
Source notes (1)
- Footnote au majeshi mawili
Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu. Copyright © 2018, 2024 Biblica, Inc. Licensed under CC BY-SA 4.0. “Biblica” ni alama ya biashara iliyosajiliwa katika United States Patent and Trademark Office (ofisi ya hataza na alama za biashara Marekani) na shirika la Biblica, Inc. Source: eBible.org. Typeset from the source files; no intended changes to scripture wording. BibleKenya is not endorsed by the rights holder.
Full source notice & licence · CC BY-SA 4.0 · SourceEdition imported 2026-10-25.