Skip to content
BibleKenya

Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu

Wimbo 4

Mpenzi

Tazama jinsi ulivyo mzuri, mpendwa wangu!

Ee, jinsi ulivyo mzuri!

Macho yako nyuma ya shela yako

ni kama ya hua.

Nywele zako ni kama kundi la mbuzi

wakishuka kutoka Mlima Gileadi.

Meno yako ni kama kundi la kondoo waliokatwa manyoya sasa hivi,

wanaotoka kuogeshwa.

Kila jino lina pacha lake;

hakuna hata moja lililo pekee.

Midomo yako ni kama uzi mwekundu,

kinywa chako kinapendeza.

Mashavu yako nyuma ya shela yako

ni kama vipande viwili vya komamanga.

Shingo yako ni kama mnara wa Daudi,

uliojengwa kwa madaha,

juu yake zimetundikwa ngao elfu,

zote ni ngao za mashujaa.

Matiti yako mawili ni kama wana-paa wawili,

kama wana-paa mapacha

wajilishao kati ya yungiyungi.

Hata kupambazuke na vivuli vikimbie,

nitaenda kwenye mlima wa manemane

na kwenye kilima cha uvumba.

Wewe ni mzuri kote, mpendwa wangu,

hakuna hitilafu ndani yako.

Nenda nami kutoka Lebanoni, bibi arusi wangu,

nenda nami kutoka Lebanoni.

Shuka kutoka ncha ya Amana,

kutoka juu ya Seniri, kilele cha Hermoni,

kutoka mapango ya simba

na kutoka mlima wapendapo kukaa chui.

Umeiba moyo wangu, dada yangu, bibi arusi wangu;

umeiba moyo wangu

kwa mtazamo mmoja wa macho yako,

kwa kito kimoja cha mkufu wako.

Tazama jinsi pendo lako linavyofurahisha,

dada yangu, bibi arusi wangu!

Pendo lako linafurahisha aje zaidi ya divai,

na harufu ya marhamu yako zaidi ya manukato yoyote!

Midomo yako inadondosha utamu kama sega la asali,

bibi arusi wangu;

maziwa na asali viko chini ya ulimi wako.

Harufu nzuri ya mavazi yako ni kama ile ya Lebanoni.

Wewe ni bustani iliyofungwa, dada yangu,

bibi arusi wangu;

wewe ni chanzo cha maji kilichozungushiwa kabisa,

chemchemi yangu peke yangu.

Mimea yako ni bustani ya mikomamanga

yenye matunda mazuri sana,

yenye hina na nardo,

nardo na zafarani,

mchai na mdalasini,

pamoja na kila aina ya mti wa uvumba,

manemane na udi,

na aina zote za vikolezo bora kuliko vyote.

Wewe ni chemchemi ya bustani,

kisima cha maji yanayotiririka,

yakitiririka kutoka Lebanoni.

Mpendwa

Amka, upepo wa kaskazini,

na uje, upepo wa kusini!

Vuma juu ya bustani yangu,

ili harufu yake nzuri iweze kuenea mpaka ng’ambo.

Mpenzi wangu na aje bustanini mwake

na kuonja matunda mazuri sana.

Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu. Copyright © 2018, 2024 Biblica, Inc. Licensed under CC BY-SA 4.0. “Biblica” ni alama ya biashara iliyosajiliwa katika United States Patent and Trademark Office (ofisi ya hataza na alama za biashara Marekani) na shirika la Biblica, Inc. Source: eBible.org. Typeset from the source files; no intended changes to scripture wording. BibleKenya is not endorsed by the rights holder.

Full source notice & licence · CC BY-SA 4.0 · SourceEdition imported 2026-10-25.

BibleKenya

Reader settings

Theme
Font
Alignment
Reading width

Saved in this browser and used offline too. Press ? for keyboard shortcuts.