Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu
Wimbo 1
Wimbo ulio bora wa Sulemani.
Mpendwa
Unibusu kwa busu la kinywa chako,
kwa maana upendo wako unafurahisha kuliko divai.
Manukato yako yananukia vizuri,
jina lako ni kama manukato yaliyomiminwa.
Ndiyo sababu wanawali wanakupenda!
Nichukue twende nawe, na tufanye haraka!
Mfalme na anilete ndani ya vyumba vyake.
Rafiki
Tunakushangilia na kukufurahia,
tutasifu upendo wako kuliko divai.
Mpendwa
Tazama jinsi ilivyo bora wakupende!
Mimi ni mweusi, lakini napendeza,
enyi binti za Yerusalemu,
mweusi kama mahema ya Kedari,
kama mapazia ya hema la Sulemani.
Usinikazie macho kwa sababu mimi ni mweusi,
kwa sababu nimefanywa mweusi na jua.
Wana wa mama yangu walinikasirikia
na kunifanya niwe mtunza mashamba ya mizabibu.
Shamba langu mwenyewe la mizabibu nimeliacha.
Niambie, wewe ninayekupenda,
unalisha wapi kundi lako la kondoo
na ni wapi unapowapumzisha kondoo wako adhuhuri.
Kwa nini niwe kama mwanamke aliyefunikwa shela
karibu na makundi ya rafiki zako?
Rafiki
Kama hujui, ewe mwanamke mzuri kuliko wote,
fuata nyayo za kondoo,
na kulisha wana-mbuzi wako
karibu na mahema ya wachungaji.
Mpenzi
Mpendwa wangu, ninakufananisha na farasi jike
aliyefungwa katika mojawapo ya magari ya vita ya Farao.
Mashavu yako yanapendeza yakiwa na vipuli,
shingo yako ikiwa na mikufu ya vito.
Tutakufanyia vipuli vya dhahabu,
vyenye kupambwa kwa fedha.
Mpendwa
Mfalme alipokuwa mezani pake,
manukato yangu yalisambaza harufu yake nzuri.
Mpenzi wangu kwangu mimi ni kifuko cha manemane
kati ya matiti yangu.
Mpenzi wangu kwangu mimi ni kama kishada cha maua ya mhina
kutoka mashamba ya mizabibu ya En-Gedi.
Mpenzi
Tazama jinsi ulivyo mzuri, mpendwa wangu!
Tazama jinsi ulivyo mzuri!
Macho yako ni kama ya hua.
Mpendwa
Tazama jinsi ulivyo mzuri, mpenzi wangu!
Ee, tazama jinsi unavyopendeza!
Na kitanda chetu ni cha majani mazuri.
Mpenzi
Nguzo za nyumba yetu ni mierezi,
na mapao yetu ni miberoshi.
Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu. Copyright © 2018, 2024 Biblica, Inc. Licensed under CC BY-SA 4.0. “Biblica” ni alama ya biashara iliyosajiliwa katika United States Patent and Trademark Office (ofisi ya hataza na alama za biashara Marekani) na shirika la Biblica, Inc. Source: eBible.org. Typeset from the source files; no intended changes to scripture wording. BibleKenya is not endorsed by the rights holder.
Full source notice & licence · CC BY-SA 4.0 · SourceEdition imported 2026-10-25.