Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu
Ufunuo 15
Malaika saba na mapigo saba
Ndipo nikaona ishara nyingine kubwa ya ajabu mbinguni: malaika saba wenye yale mapigo saba ya mwisho, kwa sababu kwa mapigo hayo ghadhabu ya Mungu ilikuwa imekamilika. Nikaona kile kilichoonekana kama bahari ya kioo iliyochanganyikana na moto. Kando ya hiyo bahari, walikuwa wamesimama wale watu waliomshinda yule mnyama na sanamu yake pamoja na tarakimu ya jina lake. Mikononi mwao walikuwa wameshika vinubi walivyopewa na Mungu. Nao wakaimba wimbo wa Musa, mtumishi wa Mungu, na wimbo wa Mwana-Kondoo, wakisema:
“Bwana Mungu Mwenyezi,
matendo yako ni makuu na ya ajabu.
Njia zako wewe ni za haki na za kweli,
Mfalme wa nyakati zote!
Ni nani ambaye hatakuogopa wewe Mwenyezi Mungu
na kulitukuza jina lako?
Kwa kuwa wewe peke yako ndiwe mtakatifu.
Mataifa yote yatakuja
na kuabudu mbele zako,
kwa kuwa matendo yako ya haki
yamedhihirishwa.”
Baada ya haya nikatazama, nalo Hekalu la Hema la Ushuhuda lilikuwa limefunguliwa mbinguni. Ndani ya lile Hekalu wakatoka malaika saba wakiwa na mapigo saba. Walikuwa wamevaa nguo safi za kitani iliyong’aa, na kufungwa mikanda ya dhahabu vifuani mwao. Ndipo mmoja wa wale viumbe wanne wenye uhai akawapa wale malaika saba mabakuli saba ya dhahabu yaliyojaa ghadhabu ya Mungu, yeye aishiye milele na milele. Nalo lile Hekalu lilijawa na moshi uliotokana na utukufu wa Mungu na uweza wake, wala hakuna yeyote aliyeweza kuingia mle Hekaluni hadi yale mapigo saba ya wale malaika saba yalipomalizika.
Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu. Copyright © 2018, 2024 Biblica, Inc. Licensed under CC BY-SA 4.0. “Biblica” ni alama ya biashara iliyosajiliwa katika United States Patent and Trademark Office (ofisi ya hataza na alama za biashara Marekani) na shirika la Biblica, Inc. Source: eBible.org. Typeset from the source files; no intended changes to scripture wording. BibleKenya is not endorsed by the rights holder.
Full source notice & licence · CC BY-SA 4.0 · SourceEdition imported 2026-10-25.