Skip to content
BibleKenya

Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu

Zaburi 73

Kitabu cha Tatu

(Zaburi 73–89)

Haki ya Mwenyezi Mungu

Zaburi ya Asafu.

Hakika Mungu ni mwema kwa Israeli,

kwa wale ambao mioyo yao ni safi.

Bali mimi, miguu yangu ilikuwa karibu kuteleza;

nilikuwa karibu kuanguka.

Kwa maana niliwaonea wivu wenye kujivuna

nilipoona kufanikiwa kwa waovu.

Wao hawana taabu;

miili yao ina afya na nguvu1.

Hawapati shida zinazowataabisha watu wengine,

wala hawapati mapigo kama wanadamu wengine.

Kwa hiyo kiburi ni mkufu wao,

wamejivika jeuri.

Uovu hutoka katika mioyo yao iliyokufa ganzi,

majivuno maovu kutoka mioyoni mwao hayana kikomo.

Hudhihaki na kusema kwa ukorofi,

katika majivuno yao wanatishia kutesa.

Vinywa vyao huweka madai hata kwa mbingu,

nazo ndimi zao humiliki duniani.

Kwa hiyo watu wao huwageukia

na kunywa maji tele2.

Wanasema, “Mungu awezaje kujua?

Je, Yeye Aliye Juu Sana anayo maarifa?”

Hivi ndivyo walivyo waovu:

siku zote hawajali,

wanaongezeka katika utajiri.

Hakika nimeuweka moyo wangu safi bure,

ni bure nimenawa mikono yangu nisiwe na hatia.

Mchana kutwa nimetaabika,

nimeadhibiwa kila asubuhi.

Kama ningesema, “Nitasema hivi,”

ningekuwa nimewasaliti watoto wako.

Nilipojaribu kuelewa haya yote,

yalikuwa magumu kwangu kuelewa.

Hadi nilipoingia patakatifu pa Mungu,

ndipo nilitambua mwisho wao.

Hakika unawaweka mahali pa utelezi,

unawaangusha chini kwa uharibifu.

Tazama jinsi wanavyoangamizwa ghafula,

wanatoweshwa kabisa na vitisho!

Kama ndoto mtu aamkapo,

hivyo wakati uinukapo, Ee Bwana,

utawatowesha kama ndoto.

Moyo wangu ulipohuzunishwa,

na roho yangu ilipotiwa uchungu,

nilikuwa mpumbavu na mjinga,

nilikuwa mnyama mkatili mbele yako.

Hata hivyo niko pamoja nawe siku zote,

umenishika mkono wangu wa kuume.

Unaniongoza kwa ushauri wako,

hatimaye utaniingiza katika utukufu.

Nani niliye naye mbinguni ila wewe?

Dunia haina chochote ninachokitamani ila wewe.

Mwili na moyo wangu vyaweza kushindwa,

bali Mungu ni nguvu ya moyo wangu

na fungu langu milele.

Wale walio mbali nawe wataangamia,

unawaangamiza wote wasio waaminifu kwako.

Lakini kwangu mimi,

ni vyema kuwa karibu na Mungu.

Nimemfanya Bwana Mungu Mwenyezi kimbilio langu;

nami nitayasimulia matendo yako yote.

Source notes (2)
  1. Footnote au hawana maumivu katika kufa kwao
  2. Footnote au na kupokea yote wasemayo

Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu. Copyright © 2018, 2024 Biblica, Inc. Licensed under CC BY-SA 4.0. “Biblica” ni alama ya biashara iliyosajiliwa katika United States Patent and Trademark Office (ofisi ya hataza na alama za biashara Marekani) na shirika la Biblica, Inc. Source: eBible.org. Typeset from the source files; no intended changes to scripture wording. BibleKenya is not endorsed by the rights holder.

Full source notice & licence · CC BY-SA 4.0 · SourceEdition imported 2026-10-25.

BibleKenya

Reader settings

Theme
Font
Alignment
Reading width

Saved in this browser and used offline too. Press ? for keyboard shortcuts.