Skip to content
BibleKenya

Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu

Zaburi 66

Kusifu Mwenyezi Mungu kwa ajili ya wema wake

Kwa mwimbishaji. Wimbo. Zaburi.

Mpigieni Mungu kelele za shangwe, dunia yote!

Imbeni utukufu wa jina lake;

mpeni sifa zake kwa utukufu!

Mwambieni Mungu, “Jinsi gani

yalivyo ya kutisha matendo yako!

Uwezo wako ni mkuu mno kiasi kwamba

adui wanajikunyata mbele zako.

Dunia yote yakusujudia,

wanakuimbia wewe sifa,

wanaliimbia sifa jina lako.”

Njooni mwone yale Mungu aliyoyatenda,

mambo ya kutisha aliyoyatenda

miongoni mwa wanadamu!

Alifanya bahari kuwa nchi kavu,

wakapita kati ya maji kwa miguu,

njooni, tumshangilie.

Yeye hutawala kwa uwezo wake milele,

macho yake huangalia mataifa yote:

waasi wasithubutu kujiinua dhidi yake.

Enyi mataifa, msifuni Mungu wetu,

sauti ya sifa yake isikike,

ameyahifadhi maisha yetu

na kuizuia miguu yetu kuteleza.

Ee Mungu, wewe ulitujaribu,

ukatusafisha kama fedha.

Umetuingiza kwenye nyavu

na umetubebesha mizigo mizito

migongoni mwetu.

Uliwaruhusu watu watukalie vichwani,

tulipita kwenye moto na kwenye maji,

lakini ulituleta kwenye nchi

iliyojaa utajiri tele.

Nitakuja hekaluni mwako na sadaka za kuteketezwa

na kukutimizia nadhiri zangu:

nadhiri ambazo midomo yangu iliahidi

na nilizotamka kwa kinywa changu

nilipokuwa katika shida.

Nitakutolea dhabihu za wanyama wanono

na sadaka za kondoo dume,

nitakutolea mafahali na mbuzi.

Njooni msikilize ninyi nyote mnaomcha Mungu,

nami niwaambie aliyonitendea.

Nilimlilia kwa kinywa changu,

sifa zake zilikuwa katika ulimi wangu.

Kama ningekuwa nimeyaficha maovu moyoni mwangu,

Bwana asingekuwa amenisikiliza;

lakini hakika Mungu amenisikiliza

na amesikia sauti yangu katika maombi.

Ahimidiwe Mungu,

ambaye hakulikataa ombi langu,

wala kunizuilia upendo wake!

Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu. Copyright © 2018, 2024 Biblica, Inc. Licensed under CC BY-SA 4.0. “Biblica” ni alama ya biashara iliyosajiliwa katika United States Patent and Trademark Office (ofisi ya hataza na alama za biashara Marekani) na shirika la Biblica, Inc. Source: eBible.org. Typeset from the source files; no intended changes to scripture wording. BibleKenya is not endorsed by the rights holder.

Full source notice & licence · CC BY-SA 4.0 · SourceEdition imported 2026-10-25.

BibleKenya

Reader settings

Theme
Font
Alignment
Reading width

Saved in this browser and used offline too. Press ? for keyboard shortcuts.