Skip to content
BibleKenya

Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu

Zaburi 45

Wimbo wa arusi ya kifalme

Kwa mwimbishaji. Mtindo wa utenzi wa “Yungiyungi”. Utenzi wa wana wa Kora. Wimbo wa arusi.

Moyo wangu umesisimuliwa na jambo jema

ninapomsimulia mfalme mabeti yangu;

ulimi wangu ni kalamu ya mwandishi stadi.

Wewe ni bora kuliko watu wengine wote

na midomo yako imepakwa neema,

kwa kuwa Mungu amekubariki milele.

Jifunge upanga wako pajani mwako, ee mwenye nguvu,

jivike fahari na utukufu.

Katika fahari yako, songa mbele kwa ushindi,

kwa ajili ya kweli, unyenyekevu na haki,

mkono wako wa kuume na uoneshe matendo ya kutisha.

Mishale yako mikali na ichome mioyo ya adui za mfalme,

mataifa na yaanguke chini ya nyayo zako.

Ee Mungu, kiti chako cha enzi

kitadumu milele na milele,

fimbo ya utawala wa haki

itakuwa fimbo ya utawala wa ufalme wako.

Unaipenda haki na kuchukia uovu;

kwa hiyo Mungu, Mungu wako,

amekuweka juu ya wenzako,

kwa kukupaka mafuta ya furaha.

Mavazi yako yote yana harufu nzuri

ya manemane, udi na mdalasini;

kutoka majumba ya kifalme

yaliyopambwa kwa pembe za ndovu,

sauti za vinanda vya nyuzi

zinakufanya ufurahi.

Binti za wafalme ni miongoni mwa wanawake wako waheshimiwa;

kuume kwako yupo bibi arusi malkia aliyevaa dhahabu ya Ofiri.

Sikiliza, ewe binti, fikiri na utege sikio:

Sahau watu wako na nyumba ya baba yako.

Mfalme ameshangazwa na uzuri wako;

mheshimu, kwa kuwa yeye ni bwana wako.

Binti Tiro atakuletea zawadi,

watu wenye utajiri watatafuta upendeleo wako.

Ufahari wote una binti mfalme katika chumba chake;

vazi lake limefumwa kwa nyuzi za dhahabu.

Anaongozwa kwa mfalme,

akiwa amevalia mavazi yaliyotariziwa,

mabikira wenzake wanamfuata

na wanaletwa kwako.

Wanaingizwa ndani kwa shangwe na furaha,

na kuingia katika jumba la mfalme.

Wana wenu watachukua nafasi za baba zenu,

mtawafanya wakuu katika nchi yote.

Nitadumisha kumbukumbu lako katika vizazi vyote,

kwa hiyo mataifa watakusifu milele na milele.

Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu. Copyright © 2018, 2024 Biblica, Inc. Licensed under CC BY-SA 4.0. “Biblica” ni alama ya biashara iliyosajiliwa katika United States Patent and Trademark Office (ofisi ya hataza na alama za biashara Marekani) na shirika la Biblica, Inc. Source: eBible.org. Typeset from the source files; no intended changes to scripture wording. BibleKenya is not endorsed by the rights holder.

Full source notice & licence · CC BY-SA 4.0 · SourceEdition imported 2026-10-25.

BibleKenya

Reader settings

Theme
Font
Alignment
Reading width

Saved in this browser and used offline too. Press ? for keyboard shortcuts.