Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu
Zaburi 36
Uovu wa mwanadamu
Kwa mwimbishaji. Zaburi ya Daudi mtumishi wa Mwenyezi Mungu.
Kuna neno moyoni mwangu
kutoka kwa Mungu
kuhusu hali ya dhambi ya mwovu.
Hakuna hofu ya Mungu
mbele ya macho yake.
Kwa kuwa machoni pake mwenyewe hujisifu mno
hata hawezi kugundua au kuichukia dhambi yake.
Maneno ya kinywa chake ni maovu na ya udanganyifu,
ameacha kuwa mwenye hekima au kutenda mema.
Hata kitandani mwake hupanga hila mbaya,
hujitia katika njia ya dhambi
na hakatai lililo baya.
Upendo wako, Ee Mwenyezi Mungu, unafika hadi mbinguni,
uaminifu wako hadi kwenye anga.
Haki yako ni kama milima mikubwa,
hukumu zako ni kama kilindi kikuu.
Ee Mwenyezi Mungu, wewe huwahifadhi
mwanadamu na mnyama.
Upendo wako usiokoma
ni wa thamani mno!
Watu wakuu na wadogo
hujificha uvulini wa mabawa yako.
Wanajifurahisha katika wingi ulio nyumbani mwako,
nawe utawanywesha katika mto wa furaha zako.
Kuwa pamoja nawe ni kijito cha uzima,
katika nuru yako twaona nuru.
Dumisha upendo wako kwa wale wanaokujua wewe,
haki yako kwa wale walio wanyofu wa moyo.
Mguu wa mwenye kiburi usije dhidi yangu,
wala mkono wa mwovu usinifukuze.
Tazama jinsi watenda maovu walivyoanguka:
wametupwa chini, hawawezi kuinuka!
Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu. Copyright © 2018, 2024 Biblica, Inc. Licensed under CC BY-SA 4.0. “Biblica” ni alama ya biashara iliyosajiliwa katika United States Patent and Trademark Office (ofisi ya hataza na alama za biashara Marekani) na shirika la Biblica, Inc. Source: eBible.org. Typeset from the source files; no intended changes to scripture wording. BibleKenya is not endorsed by the rights holder.
Full source notice & licence · CC BY-SA 4.0 · SourceEdition imported 2026-10-25.