Skip to content
BibleKenya

Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu

Zaburi 25

Kumwomba Mwenyezi Mungu uongozi na ulinzi

Zaburi ya Daudi.

Kwako wewe, Ee Mwenyezi Mungu,

naweka tumaini yangu.

Ni wewe ninayekutumainia,

Usiniache niaibike,

wala adui zangu wanishinde.

Kamwe hakuna hata mmoja anayekutegemea

atakayeaibishwa,

bali wataaibishwa

wafanyao hila bila sababu.

Nioneshe njia zako, Ee Mwenyezi Mungu,

nifundishe mapito yako,

niongoze katika kweli yako na kunifundisha,

kwa maana wewe ni Mungu Mwokozi wangu,

nalo tumaini langu liko kwako wakati wote.

Kumbuka, Ee Mwenyezi Mungu, rehema zako kuu na upendo,

kwa maana zimekuwepo tangu zamani.

Usizikumbuke dhambi za ujana wangu

wala njia zangu za uasi,

sawasawa na upendo wako unikumbuke,

kwa maana wewe ni mwema, Ee Mwenyezi Mungu.

Mwenyezi Mungu ni mwema na mwenye adili,

kwa hiyo huwafundisha wenye dhambi njia zake.

Huwaongoza wanyenyekevu katika haki,

naye huwafundisha njia yake.

Njia zote za Mwenyezi Mungu ni za upendo na uaminifu

kwa wale wanaoshika shuhuda za agano lake.

Ee Mwenyezi Mungu, kwa ajili ya jina lako,

unisamehe uovu wangu, ijapokuwa ni mwingi.

Ni nani basi, mtu yule anayemcha Mwenyezi Mungu?

Atamfundisha katika njia

atakayoichagua kwa ajili yake.

Mtu huyo atafanikiwa maishani mwake,

nao wazao wake watairithi nchi.

Siri ya Mwenyezi Mungu iko kwa wale wamchao,

yeye huwajulisha agano lake.

Macho yangu humwelekea Mwenyezi Mungu daima,

kwa kuwa yeye peke yake ndiye ataitoa

miguu yangu kutoka mtego.

Nigeukie na unihurumie,

kwa maana mimi ni mpweke na mwenye kuteseka.

Shida za moyo wangu zimeongezeka,

niokoe katika dhiki yangu.

Uangalie mateso na shida zangu

na uniondolee dhambi zangu zote.

Tazama adui zangu walivyo wengi,

pia uone jinsi wanavyonichukia vikali!

Uyalinde maisha yangu na uniokoe,

usiniache niaibike,

kwa maana nimekukimbilia wewe.

Uadilifu na uaminifu vinilinde,

kwa sababu tumaini langu ni kwako, Mwenyezi Mungu.

Ee Mungu, wakomboe Israeli,

katika shida zao zote!

Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu. Copyright © 2018, 2024 Biblica, Inc. Licensed under CC BY-SA 4.0. “Biblica” ni alama ya biashara iliyosajiliwa katika United States Patent and Trademark Office (ofisi ya hataza na alama za biashara Marekani) na shirika la Biblica, Inc. Source: eBible.org. Typeset from the source files; no intended changes to scripture wording. BibleKenya is not endorsed by the rights holder.

Full source notice & licence · CC BY-SA 4.0 · SourceEdition imported 2026-10-25.

BibleKenya

Reader settings

Theme
Font
Alignment
Reading width

Saved in this browser and used offline too. Press ? for keyboard shortcuts.