Skip to content
BibleKenya

Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu

Zaburi 147

Kumsifu Mwenyezi Mungu

Msifuni Mwenyezi Mungu.1

Tazama jinsi ilivyo vyema kumwimbia Mungu wetu sifa,

jinsi inavyopendeza na kustahili kumsifu yeye!

Mwenyezi Mungu hujenga Yerusalemu,

huwakusanya Israeli walio uhamishoni.

Anawaponya waliovunjika mioyo

na kuvifunga vidonda vyao.

Huzihesabu nyota

na huipa kila moja jina lake.

Bwana wetu ni mkuu na mwenye uwezo mwingi,

ufahamu wake hauna kikomo.

Mwenyezi Mungu huwahifadhi wanyenyekevu

lakini huwashusha waovu hadi mavumbini.

Mwimbieni Mwenyezi Mungu kwa shukrani,

mpigieni Mungu wetu kinubi.

Yeye huzifunika anga kwa mawingu,

huinyeshea ardhi mvua,

na kuzifanya nyasi kuota juu ya vilima.

Huwapa chakula mifugo

na pia makinda ya kunguru yanapolia.

Furaha yake haipo katika nguvu za farasi,

wala furaha yake kwenye miguu ya shujaa.

Mwenyezi Mungu hupendezwa na wale wamchao,

wale wanaoweka tumaini lao katika upendo wake usiokoma.

Mtukuze Mwenyezi Mungu, ee Yerusalemu,

msifu Mungu wako, ee Sayuni,

kwa maana huimarisha makomeo ya malango yako

na huwabariki watu wako walio ndani yako.

Huwapa amani mipakani mwenu

na kukushibisha kwa ngano safi kabisa.

Hutuma amri yake duniani,

neno lake hukimbia kasi.

Anatandaza theluji kama sufu

na kutawanya umande kama majivu.

Huvurumisha mvua yake ya mawe kama changarawe.

Ni nani awezaye kustahimili ukali wa baridi yake?

Hutuma neno lake na kuviyeyusha,

huvumisha upepo wake, nayo maji hutiririka.

Amemfunulia Yakobo neno lake,

sheria zake na maagizo yake kwa Israeli.

Hajafanya hivyo kwa taifa lingine lolote,

hawazijui sheria zake.

Msifuni Mwenyezi Mungu.

Source notes (1)
  1. Footnote kwa Kiebrania ni Hallelu Yah ; pia 147:20 .

Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu. Copyright © 2018, 2024 Biblica, Inc. Licensed under CC BY-SA 4.0. “Biblica” ni alama ya biashara iliyosajiliwa katika United States Patent and Trademark Office (ofisi ya hataza na alama za biashara Marekani) na shirika la Biblica, Inc. Source: eBible.org. Typeset from the source files; no intended changes to scripture wording. BibleKenya is not endorsed by the rights holder.

Full source notice & licence · CC BY-SA 4.0 · SourceEdition imported 2026-10-25.

BibleKenya

Reader settings

Theme
Font
Alignment
Reading width

Saved in this browser and used offline too. Press ? for keyboard shortcuts.