Skip to content
BibleKenya

Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu

Zaburi 116

Shukrani kwa kuokolewa kutoka mauti

Nampenda Mwenyezi Mungu kwa maana amesikia sauti yangu;

amesikia kilio changu ili anihurumie.

Kwa sababu amenitegea sikio lake,

nitamwita siku zote za maisha yangu.

Kamba za mauti zilinizunguka,

vitisho vya Kuzimu1 vilinipata,

nikalemewa na taabu na huzuni.

Ndipo nikaliitia jina la Mwenyezi Mungu:

“Ee Mwenyezi Mungu, niokoe!”

Mwenyezi Mungu ni mwenye neema na haki,

Mungu wetu ni mwingi wa huruma.

Mwenyezi Mungu huwalinda wanyenyekevu,

nilipokuwa katika shida kubwa, aliniokoa.

Ee nafsi yangu, tulia tena,

kwa kuwa Mwenyezi Mungu amekuwa mwema kwako.

Kwa kuwa wewe, Ee Mwenyezi Mungu,

umeniokoa nafsi yangu na mauti,

macho yangu kutokana na machozi,

miguu yangu kutokana na kujikwaa,

ili niweze kutembea mbele za Mwenyezi Mungu,

katika nchi ya walio hai.

Nilimwamini Mwenyezi Mungu, niliposema,

“Mimi nimeteseka sana.”

Katika taabu yangu nilisema,

“Wanadamu wote ni waongo.”

Nimrudishie Mwenyezi Mungu nini

kwa wema wake wote alionitendea?

Nitakiinua kikombe cha wokovu

na kulitangaza jina la Mwenyezi Mungu.

Nitazitimiza nadhiri zangu kwa Mwenyezi Mungu

mbele za watu wake wote.

Kifo cha watakatifu kina thamani

machoni pa Mwenyezi Mungu.

Ee Mwenyezi Mungu, hakika mimi ni mtumishi wako,

mimi ni mtumishi wako,

mwana wa mjakazi wako2;

umeniweka huru

toka katika minyororo yangu.

Nitakutolea dhabihu ya kukushukuru

na kuliita jina la Mwenyezi Mungu.

Nitazitimiza nadhiri zangu kwa Mwenyezi Mungu

mbele za watu wake wote,

katika nyua za nyumba ya Mwenyezi Mungu,

katikati yako, ee Yerusalemu.

Msifuni Mwenyezi Mungu.3

Source notes (3)
  1. Footnote Kuzimu kwa Kiebrania ni Sheol , yaani Shimo lisilo na mwisho.
  2. Footnote au mwanao mwaminifu
  3. Footnote kwa Kiebrania ni Hallelu Yah.

Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu. Copyright © 2018, 2024 Biblica, Inc. Licensed under CC BY-SA 4.0. “Biblica” ni alama ya biashara iliyosajiliwa katika United States Patent and Trademark Office (ofisi ya hataza na alama za biashara Marekani) na shirika la Biblica, Inc. Source: eBible.org. Typeset from the source files; no intended changes to scripture wording. BibleKenya is not endorsed by the rights holder.

Full source notice & licence · CC BY-SA 4.0 · SourceEdition imported 2026-10-25.

BibleKenya

Reader settings

Theme
Font
Alignment
Reading width

Saved in this browser and used offline too. Press ? for keyboard shortcuts.