Skip to content
BibleKenya

Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu

Mithali 1

Utangulizi: Kusudi na kiini

Mithali za Sulemani mwana wa Daudi, mfalme wa Israeli:

Kwa kupata hekima na nidhamu;

kwa kufahamu maneno ya busara;

kwa kujipatia nidhamu na busara,

kufanya lililo sawa, haki na bila kupendelea;

huwapa busara wajinga1,

maarifa na akili kwa vijana;

wenye hekima na wasikilize nao waongeze elimu yao,

wenye kupambanua na wapate mwongozo;

kwa kufahamu mithali na mifano,

misemo na vitendawili vya wenye hekima.

Kumcha Mwenyezi Mungu ni chanzo cha maarifa,

lakini wapumbavu2 hudharau hekima na adabu.

Maelezo juu ya hekima na upumbavu

Onyo dhidi ya ushawishi wa rafiki waovu

Mwanangu, sikiliza mwongozo wa baba yako,

wala usiyaache mafundisho ya mama yako.

Hayo yatakuwa taji la maua la neema kichwani pako,

na mkufu wa kuipamba shingo yako.

Mwanangu, wenye dhambi wakikushawishi,

usikubaliane nao.

Wakisema, “Twende tufuatane;

tukamvizie mtu na kumwaga damu,

njoo tukavizie nafsi isiyo na hatia;

tuwameze wakiwa hai kama kaburi3,

wakiwa wazima kama wale wanaotumbukia shimoni.

Tutapata aina zote za vitu vya thamani

na kujaza nyumba zetu kwa nyara.

Njoo ushirikiane nasi,

vitu vyote tutakavyopata tutagawana.”

Mwanangu, usiandamane nao.

Usiweke mguu wako katika njia zao,

kwa kuwa miguu yao hukimbilia kwenye dhambi,

ni wepesi kumwaga damu.

Tazama ni jinsi gani ilivyo kazi bure kutandaza wavu

wakati ndege wote wanakuona!

Watu hawa huvizia kumwaga damu yao wenyewe;

hujivizia tu wenyewe!

Huu ndio mwisho wa wote ambao wanajipatia mali kwa hila;

huuondoa uhai wa wale wenye mali.

Onyo dhidi ya kukataa hekima

Hekima huita kwa sauti kuu barabarani,

hupaza sauti yake kwenye viwanja vikubwa;

kwenye makutano ya barabara za mji

zenye makelele mengi hupaza sauti,

kwenye malango ya mji hutoa hotuba yake:

“Enyi wajinga, mtashikilia ujinga wenu hadi lini?

Hadi lini wenye mizaha watafurahia mizaha,

na wapumbavu kuchukia maarifa?

Kama mngekuwa mmeitikia karipio langu,

ningekuwa nimemimina roho yangu kwenu

na kuwafahamisha maneno yangu.

Lakini kwa kuwa mlinikataa nilipowaita

na hakuna yeyote aliyekubali

niliponyoosha mkono wangu,

kwa kuwa mliyapuuza mashauri yangu yote

na hamkukubali karipio langu,

mimi nami nitawacheka katika maafa yenu,

nitawadhihaki janga litakapowapata:

janga litakapowapata kama tufani,

maafa yatakapowazoa kama upepo wa kisulisuli,

dhiki na taabu zitakapowalemea.

“Ndipo watakaponiita lakini sitawajibu;

watanitafuta lakini hawatanipata.

Kwa kuwa walichukia maarifa,

wala hawakuchagua kumcha Mwenyezi Mungu,

kwa kuwa hawakukubali mashauri yangu,

na kukataa maonyo yangu,

watakula matunda ya njia zao,

na watashibishwa matunda ya hila zao.

Kwa kuwa ukaidi wa wajinga utawaua,

na kuridhika kwa wajinga kutawaangamiza.

Lakini yeyote anisikilizaye ataishi kwa usalama,

atatulia, bila kuwa na hofu ya madhara.”

Source notes (3)
  1. Footnote Neno la Kiebrania lililotafsiriwa mjinga (wingi wajinga ) linamaanisha mtu anayeamini chochote, asiye na maadili, na mwenye roho ya kutenda uovu.
  2. Footnote Neno la Kiebrania lililotafsiriwa mpumbavu (wingi wapumbavu ) linamaanisha mtu asiye na maadili.
  3. Footnote Kaburi hapa maana yake ni Kuzimu ; kwa Kiebrania ni Sheol.

Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu. Copyright © 2018, 2024 Biblica, Inc. Licensed under CC BY-SA 4.0. “Biblica” ni alama ya biashara iliyosajiliwa katika United States Patent and Trademark Office (ofisi ya hataza na alama za biashara Marekani) na shirika la Biblica, Inc. Source: eBible.org. Typeset from the source files; no intended changes to scripture wording. BibleKenya is not endorsed by the rights holder.

Full source notice & licence · CC BY-SA 4.0 · SourceEdition imported 2026-10-25.

BibleKenya

Reader settings

Theme
Font
Alignment
Reading width

Saved in this browser and used offline too. Press ? for keyboard shortcuts.