Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu
Nehemia 6
Upinzani zaidi wakati wa ujenzi
Habari zilipofika kwa Sanbalati, Tobia, Geshemu Mwarabu, na adui zetu wengine kwamba nimejenga tena ukuta na hakuna nafasi iliyobakia ndani yake, ingawa hata wakati huo sikuwa nimeweka milango kwenye malango, Sanbalati na Geshemu wakanitumia ujumbe huu: “Njoo, tukutane katika mojawapo ya vijiji katika nchi tambarare ya Ono.”
Lakini walikuwa wakikusudia kunidhuru. Kwa hiyo niliwatuma wajumbe kwao na majibu haya: “Kazi ninayoifanya ni kubwa sana, siwezi kuja. Kwa nini niiache kazi isimame nije kwenu?” Walinitumia ujumbe huo huo mara nne, na kila mara nikawapa jibu lile lile.
Basi, mara ya tano, Sanbalati akamtuma msaidizi wake kwangu akiwa na ujumbe ule ule, naye alikuwa amechukua mkononi mwake barua isiyofungwa, iliyokuwa imeandikwa:
“Habari imeenezwa miongoni mwa mataifa, naye Geshemu anasema kwamba ni kweli, kuwa wewe na Wayahudi mnapanga njama ya kuasi, ndiyo sababu mnajenga ukuta. Zaidi ya hayo, kufuatana na taarifa hizi, karibuni utakuwa mfalme wao, na hata umewateua manabii wafanye tangazo hili kukuhusu huko Yerusalemu: ‘Yuko mfalme katika Yuda!’ Sasa taarifa hii itarudishwa kwa mfalme. Basi njoo, tufanye shauri pamoja.”
Nilimpelekea jibu hili: “Hakuna jambo kama hilo unalosema linalofanyika. Unalitunga tu kwenye kichwa chako.”
Wote walikuwa wakijaribu kutuogopesha, wakifikiri hivi: “Mikono ya watu italegea kiasi kwamba hawataweza kufanya kazi, nayo haitakamilika.”
Lakini niliomba, “Ee Mungu, sasa nitie mikono yangu nguvu.”
Siku moja nilienda nyumbani mwa Shemaya mwana wa Delaya, mwana wa Mehetabeli, aliyekuwa amefungwa ndani ya nyumba yake. Akasema, “Tukutane katika nyumba ya Mungu, ndani ya Hekalu, na tufunge milango ya Hekalu, kwa sababu watu wanakuja kukuua. Naam, wanakuja usiku kukuua.”
Lakini nikasema, “Je, mtu kama mimi akimbie? Au mtu kama mimi aende Hekaluni kuokoa maisha yake? Sitaenda!” Nilitambua kwamba Mungu hakumtuma, bali alitabiri dhidi yangu kwa sababu Tobia na Sanbalati walikuwa wamemwajiri. Alikuwa ameajiriwa kunitisha ili kwa kufanya jambo hili nitende dhambi, kisha waweze kuniharibia jina langu na kuniaibisha.
Ee Mungu wangu, wakumbuke Tobia na Sanbalati kwa sababu ya yale waliyotenda. Pia kumbuka nabii mke Noadia na manabii wengine ambao wamekuwa wakijaribu kunitisha.
Upinzani baada ya ukuta kukamilika
Basi ukuta ukakamilika siku ya ishirini na tano mwezi wa Eluli1; kazi ilichukua siku hamsini na mbili. Adui zetu wote waliposikia kuhusu hili, mataifa yote yaliyotuzunguka yakaogopa na kupoteza ujasiri, kwa sababu yalitambua kuwa kazi hii imefanyika kwa msaada wa Mungu wetu.
Pia katika siku hizo wakuu wa Yuda walikuwa wakituma barua nyingi kwa Tobia, nayo majibu yaliyotoka kwa Tobia yaliendelea kuwajia. Kwa kuwa watu wengi katika Yuda walikuwa wamemwapia Tobia, kwani alikuwa mkwewe Shekania mwana wa Ara, na Yehohanani mwanawe alikuwa amemwoa binti Meshulamu mwana wa Berekia. Zaidi ya hayo, walikuwa wakiniarifu jinsi Tobia alivyo mtu mwema, nao walimwambia kila kitu nilichosema. Naye Tobia alituma barua za kunitisha.
Source notes (1)
- Footnote mwezi wa sita katika kalenda ya Kiyahudi
Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu. Copyright © 2018, 2024 Biblica, Inc. Licensed under CC BY-SA 4.0. “Biblica” ni alama ya biashara iliyosajiliwa katika United States Patent and Trademark Office (ofisi ya hataza na alama za biashara Marekani) na shirika la Biblica, Inc. Source: eBible.org. Typeset from the source files; no intended changes to scripture wording. BibleKenya is not endorsed by the rights holder.
Full source notice & licence · CC BY-SA 4.0 · SourceEdition imported 2026-10-25.