Skip to content
BibleKenya

Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu

Nehemia 1

Maombi ya Nehemia

Maneno ya Nehemia mwana wa Hakalia:

Katika mwezi wa Kislevu1 katika mwaka wa ishirini, wakati nilikuwa ngomeni katika jumba la kifalme la Shushani, Hanani, mmoja wa ndugu zangu, alikuja kutoka Yuda akiwa na watu wengine, nami nikawauliza kuhusu mabaki ya Wayahudi wale walionusurika kwenda uhamishoni na pia kuhusu Yerusalemu.

Wakaniambia, “Wale walionusurika kwenda uhamishoni, wale ambao wamerudi kwenye lile jimbo, wako katika taabu kubwa na aibu. Ukuta wa Yerusalemu umebomoka, na malango yake yamechomwa moto.”

Niliposikia mambo haya, niliketi, nikalia. Kwa siku kadhaa niliomboleza na kufunga na kuomba mbele za Mungu wa mbinguni. Kisha nikasema:

“Ee Mwenyezi Mungu, Mungu wa mbinguni, mkuu na mwenye kuogofya, ambaye hulishika agano lake la upendo na wale wanaompenda na kutii amri zake, tega masikio yako, na ufungue macho yako, ili usikie maombi ya mtumishi wako anayoomba mbele yako usiku na mchana kwa ajili ya watumishi wako, watu wa Israeli. Ninaungama dhambi zetu sisi Waisraeli, pamoja na zangu na za nyumba ya baba yangu, tulizotenda dhidi yako. Tumetenda uovu sana mbele zako. Hatukutii amri, maagizo na sheria ulizompa Musa mtumishi wako.

“Kumbuka agizo ulilompa Musa mtumishi wako, ukisema, ‘Mkikosa uaminifu, nitawatawanya miongoni mwa mataifa, lakini mkinirudia na kutii amri zangu, ndipo hata kama watu wenu walio uhamishoni katika miisho ya dunia, nitawakusanya kutoka huko na kuwaleta mahali nilipopachagua kuwa makao kwa ajili ya Jina langu.’

“Hawa ni watumishi wako na watu wako, uliowakomboa kwa nguvu zako kuu na mkono wako wenye nguvu. Ee Bwana, tega sikio lako na usikie maombi ya huyu mtumishi wako, na maombi ya watumishi wako wanaofurahia kuliheshimu Jina lako. Nipe leo, mimi mtumishi wako, mafanikio kwa kunipa kibali mbele ya mtu huyu.”

Kwa maana nilikuwa mnyweshaji wa mfalme.

Source notes (1)
  1. Footnote mwezi wa tisa katika kalenda ya Kiyahudi

Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu. Copyright © 2018, 2024 Biblica, Inc. Licensed under CC BY-SA 4.0. “Biblica” ni alama ya biashara iliyosajiliwa katika United States Patent and Trademark Office (ofisi ya hataza na alama za biashara Marekani) na shirika la Biblica, Inc. Source: eBible.org. Typeset from the source files; no intended changes to scripture wording. BibleKenya is not endorsed by the rights holder.

Full source notice & licence · CC BY-SA 4.0 · SourceEdition imported 2026-10-25.

BibleKenya

Reader settings

Theme
Font
Alignment
Reading width

Saved in this browser and used offline too. Press ? for keyboard shortcuts.