Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu
Walawi 27
Kukomboa kile kilicho cha Mwenyezi Mungu
Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, “Sema na Waisraeli uwaambie: ‘Kama mtu yeyote ataweka nadhiri maalum ili kuweka watu wakfu kwa Mwenyezi Mungu, kwa kutoa kiasi cha thamani inayolingana, thamani ya kukomboa mwanaume mwenye kati ya umri wa miaka ishirini na miaka sitini itakuwa shekeli hamsini1 za fedha, kulingana na shekeli ya mahali patakatifu; ikiwa ni mwanamke, weka thamani yake kwa shekeli thelathini2. Kama ni mtu mwenye umri wa miaka kati ya mitano na ishirini, weka thamani ya mwanaume kuwa shekeli ishirini3, na mwanamke shekeli kumi4. Kama ni mtu mwenye umri kati ya mwezi mmoja na miaka mitano, weka thamani ya mwanaume kuwa shekeli tano za fedha, na ile ya mwanamke kuwa shekeli tatu5 za fedha. Kama ni mtu mwenye miaka sitini na zaidi, weka thamani ya mwanaume kuwa shekeli kumi na tano6, na mwanamke shekeli kumi. Kama mtu yeyote anayeweka nadhiri ni maskini mno kuweza kulipa kiasi kilichowekwa, atampeleka huyo mtu kwa kuhani, ambaye ataweka thamani yake kulingana na kile yule anayeweka nadhiri anaweza kulipa.
“ ‘Kama kile mtu alichokiwekea nadhiri ni mnyama anayekubalika kama sadaka kwa Mwenyezi Mungu, mnyama huyo aliyetolewa kwa Mwenyezi Mungu anakuwa mtakatifu. Mtu haruhusiwi kumbadilisha au kutoa mnyama mzuri kwa mbaya, au mnyama mbaya kwa mzuri. Kama atatoa mnyama badala ya mwingine, wanyama wote wawili, yaani yule aliyetolewa na yule aliyebadiliwa, ni watakatifu. Kama alichokiwekea nadhiri ni mnyama aliye najisi, yaani yule asiyekubalika kuwa sadaka kwa Mwenyezi Mungu, huyo mnyama lazima aletwe kwa kuhani, ambaye ataamua ubora wa mnyama huyo, kama ni mzuri au mbaya. Thamani yoyote atakayoweka kuhani, hivyo ndivyo itakavyokuwa. Kama mwenye mnyama atapenda kumkomboa mnyama huyo, lazima aongeze sehemu ya tano ya thamani yake.
“ ‘Kama mtu ataweka nyumba yake wakfu kama kitu kitakatifu kwa Mwenyezi Mungu, kuhani ataamua ubora wa nyumba hiyo, kama ni nzuri au mbaya. Thamani yoyote kuhani atakayoweka, basi hivyo ndivyo itakavyokuwa. Kama mtu aliyeweka nyumba yake wakfu ataikomboa, lazima aongeze sehemu ya tano ya thamani yake, nayo nyumba itakuwa yake tena.
“ ‘Ikiwa mtu ataweka sehemu ya ardhi ya jamaa yake wakfu kwa Mwenyezi Mungu, thamani yake itawekwa kulingana na kiasi cha mbegu inayohitajiwa kupandwa katika ardhi hiyo, yaani homeri7 moja ya mbegu za shayiri kwa shekeli hamsini za fedha. Akiweka shamba lake wakfu katika Mwaka wa Yubile, ile thamani iliyokwisha wekwa itakuwa hiyo hiyo. Lakini akiliweka shamba lake wakfu baada ya Yubile, kuhani ataweka thamani kulingana na idadi ya miaka iliyobaki kufikia Mwaka wa Yubile unaofuata, na thamani yake iliyoamuliwa itapunguzwa. Kama mtu anayeweka wakfu shamba anataka kulikomboa, lazima aongeze sehemu ya tano ya thamani yake, nalo shamba litakuwa lake tena. Kama pengine halikomboi shamba hilo, au kama ameliuza kwa mtu mwingine, kamwe haliwezi kukombolewa. Shamba hilo litakapoachiwa Mwaka wa Yubile, litakuwa takatifu, kama shamba lililotolewa kwa Mwenyezi Mungu, nalo litakuwa mali ya makuhani.
“ ‘Kama mtu ameweka wakfu kwa Mwenyezi Mungu shamba alilonunua, ambalo si sehemu ya ardhi ya jamaa yake, kuhani ataamua thamani yake hadi Mwaka wa Yubile, naye huyo mtu lazima alipe thamani yake siku hiyo kama kitu kitakatifu kwa Mwenyezi Mungu. Katika Mwaka wa Yubile, shamba litarudishwa kwa mtu yule ambaye lilinunuliwa kutoka kwake, yule ambaye ardhi ilikuwa mali yake. Kila thamani lazima iwekwe kulingana na shekeli ya mahali patakatifu8: gera ishirini kwa shekeli.
“ ‘Hata hivyo, hakuna mtu atakayemweka wakfu mzaliwa wa kwanza wa mnyama, kwa kuwa mzaliwa wa kwanza tayari ni mali ya Mwenyezi Mungu; awe ng’ombe au kondoo, ni wa Mwenyezi Mungu. Kama ni mmoja wa wanyama walio najisi, aweza kumnunua kwa bei iliyowekwa, akiongeza sehemu ya tano ya thamani yake. Kama hatamkomboa, mnyama huyo atauzwa kwa bei iliyowekwa.
“ ‘Lakini chochote kile mtu alicho nacho na akakiweka wakfu9 kwa Mwenyezi Mungu, iwe ni binadamu, au mnyama, au ardhi ya jamaa, hakiwezi kuuzwa au kukombolewa. Chochote kilichowekwa wakfu ni kitakatifu sana kwa Mwenyezi Mungu.
“ ‘Mtu yeyote aliyewekwa wakfu ili kuangamizwa, hawezi kukombolewa. Mtu kama huyo lazima auawe.
“ ‘Zaka ya kila kitu kutoka shambani, iwe ni nafaka kutoka kwa ardhi, au tunda kutoka kwa miti, ni mali ya Mwenyezi Mungu; ni takatifu kwa Mwenyezi Mungu. Kama mtu akikomboa chochote cha zaka yake, lazima aongeze sehemu ya tano ya thamani yake. Zaka yote ya kundi la ng’ombe au la kondoo na mbuzi, kila mnyama wa kumi apitaye chini ya fimbo ya yule awachungaye, atakuwa kitu kitakatifu kwa Mwenyezi Mungu. Yule mnyama wa kumi hatachaguliwa kwa kigezo cha uzuri au ubaya, naye haruhusiwi kubadiliwa. Akimbadili, basi mnyama yule wa kwanza na huyo aliyebadiliwa wote watahesabiwa kuwa watakatifu, na haiwezekani kuwakomboa.’ ”
Haya ndio maagizo Mwenyezi Mungu aliyompa Musa juu ya Mlima Sinai kwa ajili ya Waisraeli.
Source notes (9)
- Footnote Shekeli 50 za fedha ni sawa na gramu 600.
- Footnote Shekeli 30 za fedha ni sawa na gramu 360.
- Footnote Shekeli 20 za fedha ni sawa na gramu 240.
- Footnote Shekeli 10 za fedha ni sawa na gramu 120.
- Footnote Shekeli tatu za fedha ni sawa na gramu 36.
- Footnote Shekeli 15 za fedha ni sawa na gramu 180.
- Footnote Homeri moja ni sawa na efa 10, ambazo ni sawa na kilo 100.
- Footnote Shekeli moja ya mahali patakatifu ni sawa na gramu 11.
- Footnote akakiweka wakfu ina maana ya kumpa Mwenyezi Mungu kabisa, daima, bila kurudiwa.
Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu. Copyright © 2018, 2024 Biblica, Inc. Licensed under CC BY-SA 4.0. “Biblica” ni alama ya biashara iliyosajiliwa katika United States Patent and Trademark Office (ofisi ya hataza na alama za biashara Marekani) na shirika la Biblica, Inc. Source: eBible.org. Typeset from the source files; no intended changes to scripture wording. BibleKenya is not endorsed by the rights holder.
Full source notice & licence · CC BY-SA 4.0 · SourceEdition imported 2026-10-25.