Skip to content
BibleKenya

Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu

Yoshua 5

Basi wafalme wote wa Waamori magharibi mwa Yordani na wafalme wote wa Kanaani waliokuwa kwenye pwani waliposikia jinsi Mwenyezi Mungu alivyoukausha Mto Yordani mbele ya Waisraeli hata tulipokwisha kuvuka, mioyo yao ikayeyuka kwa hofu, wala hawakuwa na ujasiri tena wa kukabiliana na Waisraeli.

Tohara huko Gilgali

Wakati huo Mwenyezi Mungu akamwambia Yoshua, “Tengeneza visu vya gumegume na uwatahiri Waisraeli tena.” Kwa hiyo Yoshua akatengeneza visu vya gumegume na kutahiri Waisraeli huko Gibeath-Haaralothi1.

Hii ndiyo sababu ya Yoshua kufanya hivyo: Wanaume wote waliotoka Misri, wote wenye umri wa kwenda vitani, walikufa jangwani wakiwa njiani baada ya kuondoka Misri. Watu wote waliotoka Misri walikuwa wametahiriwa, lakini watu wote waliozaliwa jangwani wakiwa safarini kutoka Misri hawakuwa wametahiriwa. Waisraeli walitembea jangwani miaka arobaini hadi wanaume wote wale waliokuwa na umri wa kwenda vitani wakati waliondoka Misri walipokwisha kufa, kwa kuwa hawakumtii Mwenyezi Mungu. Kwa maana Mwenyezi Mungu alikuwa amewaapia kuwa wasingeweza kuona nchi ambayo alikuwa amewaahidi baba zao katika kuapa kutupatia, nchi inayotiririka maziwa na asali. Kwa hiyo akawainua wana wao baada yao na hawa ndio hao ambao Yoshua aliwatahiri. Walikuwa hawajatahiriwa bado kwa sababu walikuwa safarini. Baada ya taifa lote kutahiriwa, waliendelea kukaa kambini hadi walipopona.

Mwenyezi Mungu akamwambia Yoshua, “Leo nimeiondoa aibu ya Wamisri kutoka kwenu.” Basi mahali pale pakaitwa Gilgali hadi leo.

Jioni ya siku ya kumi na nne ya mwezi, wakiwa wamepiga kambi huko Gilgali kwenye nchi tambarare za Yeriko, Waisraeli wakaadhimisha Pasaka. Siku iliyofuata Pasaka, katika siku ile ile, wakala mazao ya nchi: mikate isiyotiwa chachu na nafaka za kukaanga. Mana ilikoma siku iliyofuata baada ya Waisraeli kula chakula kilichotoka katika nchi; hapakuwa na mana tena kwa ajili ya Waisraeli, ila mwaka huo walikula mazao ya nchi ya Kanaani.

Jemadari wa jeshi la Mwenyezi Mungu

Basi Yoshua alipokuwa karibu na Yeriko, akainua macho, akaona mtu aliyesimama mbele yake, akiwa na upanga mkononi. Yoshua akamwendea na kumuuliza, “Je, wewe uko upande wetu au upande wa adui zetu?”

Akajibu, “La, siko upande wowote, lakini mimi nimekuja nikiwa jemadari wa jeshi la Mwenyezi Mungu.” Yoshua akasujudu, uso wake ukigusa chini, akamuuliza, “Je, Bwana, una ujumbe gani kwa mtumishi wako?” Jemadari wa jeshi la Mwenyezi Mungu akajibu, “Vua viatu vyako, kwa maana mahali uliposimama ni patakatifu.” Naye Yoshua akafanya hivyo.

Source notes (1)
  1. Footnote maana yake Kilima cha magovi

Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu. Copyright © 2018, 2024 Biblica, Inc. Licensed under CC BY-SA 4.0. “Biblica” ni alama ya biashara iliyosajiliwa katika United States Patent and Trademark Office (ofisi ya hataza na alama za biashara Marekani) na shirika la Biblica, Inc. Source: eBible.org. Typeset from the source files; no intended changes to scripture wording. BibleKenya is not endorsed by the rights holder.

Full source notice & licence · CC BY-SA 4.0 · SourceEdition imported 2026-10-25.

BibleKenya

Reader settings

Theme
Font
Alignment
Reading width

Saved in this browser and used offline too. Press ? for keyboard shortcuts.