Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu
Yona 3
Yona aenda Ninawi
Ndipo neno la Mwenyezi Mungu likamjia Yona mara ya pili: “Ondoka uende katika mji mkubwa wa Ninawi, ukautangazie ujumbe ninaokupa.”
Yona akalitii neno la Mwenyezi Mungu naye akaenda Ninawi. Basi Ninawi ulikuwa mji maarufu sana, ilichukua siku tatu kuuzunguka. Siku ya kwanza, Yona aliingia mjini. Akatangaza: “Baada ya siku arobaini Ninawi utaangamizwa.” Watu wa Ninawi wakamwamini Mungu, wakatangaza kufunga, watu wote kuanzia mkubwa sana hadi yule mdogo kabisa, wakavaa gunia.
Habari zilipomfikia mfalme wa Ninawi, aliondoka kwenye kiti chake cha utawala, akavua majoho yake ya mfalme, akajifunika gunia na kuketi mavumbini. Ndipo akatoa tangazo katika Ninawi yote:
“Kwa amri ya mfalme na wakuu wake:
“Msiruhusu mtu yeyote au mnyama, makundi ya ng’ombe au wanyama wengine wafugwao, kuonja kitu chochote, msiwaruhusu kula wala kunywa. Bali wanadamu na wanyama wavae gunia. Kila mmoja afanye hima kumwomba Mungu. Waziache njia zao mbaya na udhalimu ulio mikononi mwao. Ni nani ajuaye? Huenda Mungu akaghairi kwa huruma yake akaacha hasira yake kali ili tusiangamie.”
Mungu alipoona walivyofanya na jinsi walivyogeuka kutoka njia zao mbaya, akawa na huruma wala hakuleta maangamizi juu yao kama alivyokuwa ameonya.
Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu. Copyright © 2018, 2024 Biblica, Inc. Licensed under CC BY-SA 4.0. “Biblica” ni alama ya biashara iliyosajiliwa katika United States Patent and Trademark Office (ofisi ya hataza na alama za biashara Marekani) na shirika la Biblica, Inc. Source: eBible.org. Typeset from the source files; no intended changes to scripture wording. BibleKenya is not endorsed by the rights holder.
Full source notice & licence · CC BY-SA 4.0 · SourceEdition imported 2026-10-25.