Skip to content
BibleKenya

Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu

Ayubu 6

Hotuba ya pili ya Ayubu

Ayubu anajibu: Malalamiko yangu ni ya haki

Kisha Ayubu akajibu:

“Laiti uchungu wangu ungeweza kupimwa,

nayo taabu yangu yote ingewekwa kwenye mizani!

Kwa kuwa hakika ingekuwa nzito kuliko mchanga wa bahari zote,

kwa hiyo si ajabu maneno yangu yamekuwa ya haraka.

Mishale ya Mwenyezi iko ndani yangu,

roho yangu inakunywa sumu yake;

vitisho vya Mungu vimejipanga dhidi yangu.

Je, punda-mwitu hulia akiwa na majani,

au fahali hulia akiwa na chakula?

Je, chakula kisicho na ladha huliwa bila chumvi,

au upo utamu katika ute mweupe wa yai?

Ninakataa kuvigusa;

vyakula vya aina hii hunichukiza.

“Laiti ningepata haja yangu,

kwamba Mungu angenijalia hilo nililotarajia,

kwamba Mungu angekuwa radhi kuniponda,

kuuachia mkono wake na kunikatilia mbali!

Ndipo bado ningekuwa na hii faraja,

furaha yangu katika maumivu makali:

kwamba sikuwa nimeyakana maneno yake yeye Aliye Mtakatifu.

“Nina nguvu gani, hata niendelee kutumaini?

Matazamio yangu ni nini,

hata niendelee kuwa mvumilivu?

Je, mimi nina nguvu za jiwe?

Je, mwili wangu ni shaba?

Je, ninao uwezo wowote wa kujisaidia mimi mwenyewe,

wakati mafanikio yamefukuziwa mbali nami?

“Mtu anayekata tamaa angetazamia moyo wa kujitoa wa rafiki zake,

hata akiacha uchaji wa Mwenyezi.

Lakini ndugu zangu sio wa kutegemewa,

ni kama vijito vya msimu,

ni kama vijito ambavyo hufurika

wakati vimefunikwa barafu iyeyukayo,

ambavyo hujazwa na theluji inayoyeyuka,

lakini hukauka majira ya ukame,

na wakati wa hari hutoweka katika mikondo yake.

Misafara hugeuka kutoka njia zake;

hukwea kwenda kwenye nchi ya ukiwa na kuangamia.

Misafara ya Tema inatafuta maji,

wafanyabiashara wa Sheba wanaosafiri

hutazama kwa matarajio.

Wamedhikika, kwa sababu walikuwa na matumaini;

wanafika huko, lakini wanahuzunika

kwa kukosa walichotarajia.

Sasa nanyi mmethibitika

kwamba hamna msaada wowote;

mnaona jambo la kutisha,

nanyi mnaogopa.

Je, nimewahi kusema, ‘Toeni kitu kwa ajili yangu,

au mnilipie fidia kutoka mali yenu,

au niokoeni mikononi mwa adui,

au nikomboeni kutoka makucha ya wasio na huruma’?

“Nifundisheni, nami nitakaa kimya;

nionesheni nilikokosea.

Tazama yalivyo ya kuumiza maneno ya kweli!

Lakini mabishano yenu yanathibitisha nini?

Je, mna maana ya kuyasahihisha ninayosema,

na kuyafanya maneno ya mtu anayekata tamaa kama upepo?

Mngeweza hata kupiga kura kwa ajili ya yatima,

na kubadilishana rafiki yenu na mali.

“Lakini sasa kuweni na huruma mkaniangalie mimi.

Je, ningeweza kusema uongo mbele zenu?

Tulizeni hasira, msiwe wadhalimu;

angalieni tena, kwa maana nimehatarisha uadilifu wangu1.

Je, pana uovu wowote mdomoni mwangu?

Je, kinywa changu hakiwezi kupambanua hila?

Source notes (1)
  1. Footnote au haki yangu bado inasimama

Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu. Copyright © 2018, 2024 Biblica, Inc. Licensed under CC BY-SA 4.0. “Biblica” ni alama ya biashara iliyosajiliwa katika United States Patent and Trademark Office (ofisi ya hataza na alama za biashara Marekani) na shirika la Biblica, Inc. Source: eBible.org. Typeset from the source files; no intended changes to scripture wording. BibleKenya is not endorsed by the rights holder.

Full source notice & licence · CC BY-SA 4.0 · SourceEdition imported 2026-10-25.

BibleKenya

Reader settings

Theme
Font
Alignment
Reading width

Saved in this browser and used offline too. Press ? for keyboard shortcuts.