Skip to content
BibleKenya

Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu

Ayubu 23

Hotuba ya nane ya Ayubu

Ayubu anajibu: Nalalamika kwa uchungu

Ndipo Ayubu akajibu:

“Hata leo malalamiko yangu ni ya uchungu;

mkono wake ni mzito juu yangu hata nikiugua.

Laiti ningefahamu mahali pa kumwona;

laiti ningeweza kwenda mahali akaapo!

Ningeleta kesi yangu mbele zake,

na kukijaza kinywa changu na hoja.

Ningejua kwamba angenijibu nini,

na kuelewa lile angeniambia.

Je, angenipinga kwa nguvu nyingi?

La, hangenigandamiza.

Hapo mtu mwadilifu angeleta kesi yake mbele zake,

nami ningeokolewa milele na mhukumu wangu.

“Lakini nikienda mashariki, hayupo;

nikienda magharibi, simpati.

Anapokuwa kazini pande za kaskazini, simwoni;

akigeukia kusini, nako simwoni hata kidogo.

Lakini anaijua njia niiendeayo;

akiisha kunijaribu, nitatoka kama dhahabu.

Nyayo zangu zimefuata hatua zake kwa karibu;

nimeishika njia yake bila kukengeuka.

Sijaziacha amri zilizotoka mdomoni mwake;

nimeyathamini maneno ya kinywa chake

kuliko chakula changu cha kila siku.

“Lakini yeye husimama peke yake; ni nani awezaye kumpinga?

Yeye hufanya lolote atakalo.

Hutimiliza maagizo yake dhidi yangu,

na bado anayo mipango mingi kama hiyo ambayo ameiweka akiba.

Hiyo ndiyo sababu ninaingiwa na hofu mbele zake;

nifikiriapo haya yote ninamwogopa.

Mungu ameufanya moyo wangu kuzimia;

yeye Mwenyezi amenitia hofu.

Hata hivyo sijanyamazishwa na giza,

wala kwa giza nene linalofunika uso wangu.

Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu. Copyright © 2018, 2024 Biblica, Inc. Licensed under CC BY-SA 4.0. “Biblica” ni alama ya biashara iliyosajiliwa katika United States Patent and Trademark Office (ofisi ya hataza na alama za biashara Marekani) na shirika la Biblica, Inc. Source: eBible.org. Typeset from the source files; no intended changes to scripture wording. BibleKenya is not endorsed by the rights holder.

Full source notice & licence · CC BY-SA 4.0 · SourceEdition imported 2026-10-25.

BibleKenya

Reader settings

Theme
Font
Alignment
Reading width

Saved in this browser and used offline too. Press ? for keyboard shortcuts.