Skip to content
BibleKenya

Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu

Ayubu 16

Hotuba ya tano ya Ayubu

Ayubu anajibu: Hakika sina hatia

Kisha Ayubu akajibu:

“Nimepata kusikia mambo mengi kama haya,

nanyi nyote ni wafariji wenye kutaabisha!

Je, maneno yenu mengi yasiyo na maana hayana mwisho?

Mna nini hata mwendelee kushindana kwa maneno?

Mimi pia ningeweza kuzungumza kama ninyi,

kama mngekuwa katika hali yangu;

ningeweza kutoa hotuba nzuri dhidi yenu,

na kuwatikisia ninyi kichwa changu.

Lakini kinywa changu kingewatia moyo;

faraja kutoka mdomoni mwangu ingewaletea nafuu.

“Lakini nikisema, maumivu yangu bado hayatulizwi;

na nikijizuia, bado hayaondoki.

Ee Mungu, hakika umenichakaza;

umewaangamiza kabisa watu wa nyumbani mwangu wote.

Umenikunjakunja, nalo limekuwa ushahidi;

nako kukonda kwangu kumeongezeka sana na kushuhudia dhidi yangu.

Mungu amenishambulia na kunirarua katika hasira yake,

na kunisagia meno yake;

adui yangu hunikazia macho yake makali.

Watu wamenifumbulia vinywa vyao kunidhihaki;

hunipiga shavuni mwangu kwa dharau,

na kuungana pamoja dhidi yangu.

Mungu amenigeuzia kwa watu wapotovu,

na kunitupa katika makucha ya waovu.

Mambo yote yalikuwa mazuri, lakini alinivunjavunja;

amenikamata shingo na kuniponda.

Amenifanya mimi kuwa shabaha yake;

wapiga upinde wake wananizunguka.

Bila huruma, huchoma figo zangu,

na kuimwaga nyongo yangu juu ya nchi.

Huniponda tena na tena;

hunishambulia kama shujaa wa vita.

“Nimejishonea gunia juu ya mwili wangu,

nami nimezika paji la uso wangu kwenye vumbi.

Uso wangu umekuwa mwekundu kwa kulia,

macho yangu yamepigwa na giza.

Hata hivyo mikono yangu haijafanya jeuri,

na maombi yangu ni safi.

“Ee nchi, usiifunike damu yangu,

nacho kilio changu kisinyamazishwe kamwe.

Hata sasa shahidi wangu yuko mbinguni;

wakili wangu yuko juu.

Mwombezi wangu ni rafiki yangu

macho yangu yanapomwaga machozi kwa Mungu;

kwa niaba ya mtu anamsihi Mungu

kama mtu anavyosihi kwa ajili ya rafiki yake.

“Ni miaka michache tu itapita

kabla sijaenda safari ambayo sitarudi.

Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu. Copyright © 2018, 2024 Biblica, Inc. Licensed under CC BY-SA 4.0. “Biblica” ni alama ya biashara iliyosajiliwa katika United States Patent and Trademark Office (ofisi ya hataza na alama za biashara Marekani) na shirika la Biblica, Inc. Source: eBible.org. Typeset from the source files; no intended changes to scripture wording. BibleKenya is not endorsed by the rights holder.

Full source notice & licence · CC BY-SA 4.0 · SourceEdition imported 2026-10-25.

BibleKenya

Reader settings

Theme
Font
Alignment
Reading width

Saved in this browser and used offline too. Press ? for keyboard shortcuts.