Skip to content
BibleKenya

Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu

Yeremia 10

Mwenyezi Mungu na sanamu

Sikieni lile Mwenyezi Mungu anasema nanyi, ee nyumba ya Israeli. Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu:

“Usijifunze njia za mataifa

wala usitishwe na ishara katika anga,

ingawa mataifa yanatishwa nazo.

Kwa maana desturi za mataifa hazina maana,

wanakata mti msituni,

na fundi anauchonga kwa patasi.

Wanauremba kwa fedha na dhahabu,

wanaukaza kwa nyundo na misumari ili usitikisike.

Sanamu zao ni kama kinyago

kilichowekwa katika shamba la matango kutishia ndege,

nazo haziwezi kuongea;

na kwa kuwa haziwezi kutembea zinabebwa.

Usiziogope. Haziwezi kudhuru

wala kutenda lolote jema.”

Hakuna aliye kama wewe, Ee Mwenyezi Mungu;

wewe ni mkuu,

jina lako ni lenye nguvu na uweza.

Ni nani ambaye haimpasi kukuheshimu wewe,

Ee Mfalme wa mataifa?

Hii ni stahili yako.

Miongoni mwa watu wote wenye hekima

katika mataifa na katika falme zao zote,

hakuna aliye kama wewe.

Wote hawana akili, tena ni wapumbavu;

wanafundishwa na sanamu batili za miti.

Huleta fedha iliyofuliwa kutoka Tarshishi

na dhahabu kutoka Ufazi.

Kile ambacho fundi na sonara wametengeneza

huvikwa mavazi ya rangi ya samawi na urujuani:

vyote vikiwa vimetengenezwa

na mafundi stadi.

Lakini Mwenyezi Mungu ni Mungu wa kweli,

yeye ndiye Mungu aliye hai, Mfalme wa milele.

Anapokasirika, dunia hutetemeka,

mataifa hayawezi kustahimili hasira yake.

“Waambie hivi: ‘Miungu hii, ambayo haikuumba mbingu na dunia, itaangamia duniani na chini ya mbingu.’ ”

Lakini Mungu aliiumba dunia kwa uweza wake,

akaweka misingi ya ulimwengu kwa hekima yake,

na akazitandaza mbingu kwa ufahamu wake.

Atoapo sauti yake, maji yaliyo katika mbingu hunguruma;

huyafanya mawingu yainuke kutoka miisho ya dunia.

Hupeleka miali ya radi pamoja na mvua,

naye huuleta upepo kutoka ghala zake.

Kila mtu ni mjinga na hana maarifa;

kila sonara ameaibishwa na sanamu zake.

Vinyago vyake ni vya udanganyifu;

havina pumzi.

Ni ubatili tu, vitu vya kufanyia mzaha;

wakati wa hukumu yao, wataangamia.

Yeye aliye Fungu la Yakobo sivyo alivyo,

kwani ndiye Muumba wa vitu vyote,

pamoja na Israeli, kabila la urithi wake:

Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni ndilo jina lake.

Maangamizi yajayo

Kusanyeni mali na vitu vyenu mwondoke nchi hii,

enyi mnaoishi katika hali ya kuzingirwa na jeshi.

Kwa kuwa hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu:

“Wakati huu, nitawatupa nje kwa nguvu

wote wanaoishi katika nchi hii;

nitawataabisha

ili wapate kutekwa.”

Ole wangu mimi kwa ajili ya kuumia kwangu!

Jeraha langu ni kubwa!

Lakini nilisema,

“Kweli hii ni adhabu yangu,

nami sharti niistahimili.”

Hema langu limeangamizwa;

kamba zake zote zimekatwa.

Wana wangu wametekwa na hawapo tena;

hakuna hata mmoja aliyebaki wa kusimamisha hema langu

wala wa kusimamisha kibanda changu.

Wachungaji hawana akili

wala hawamuulizi Mwenyezi Mungu,

hivyo hawastawi

na kundi lao lote la kondoo limetawanyika.

Sikilizeni! Taarifa inakuja:

ghasia kubwa kutoka nchi ya kaskazini!

Hii itafanya miji ya Yuda ukiwa,

na kuwa makao ya mbweha.

Maombi ya Yeremia

Ninajua, Ee Mwenyezi Mungu, kwamba maisha ya mwanadamu si yake mwenyewe;

hawezi kuziongoza hatua zake mwenyewe.

Unirudi, Ee Mwenyezi Mungu, lakini kwa kipimo cha haki:

si katika hasira yako,

usije ukaniangamiza.

Umwage ghadhabu yako juu ya mataifa

wasiokujua wewe,

juu ya mataifa wasioliitia jina lako.

Kwa kuwa wamemwangamiza Yakobo;

wamemwangamiza kabisa

na kuiharibu nchi yake.

Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu. Copyright © 2018, 2024 Biblica, Inc. Licensed under CC BY-SA 4.0. “Biblica” ni alama ya biashara iliyosajiliwa katika United States Patent and Trademark Office (ofisi ya hataza na alama za biashara Marekani) na shirika la Biblica, Inc. Source: eBible.org. Typeset from the source files; no intended changes to scripture wording. BibleKenya is not endorsed by the rights holder.

Full source notice & licence · CC BY-SA 4.0 · SourceEdition imported 2026-10-25.

BibleKenya

Reader settings

Theme
Font
Alignment
Reading width

Saved in this browser and used offline too. Press ? for keyboard shortcuts.