Skip to content
BibleKenya

Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu

Isaya 58

Mfungo wa kweli

“Piga kelele, usizuie.

Paza sauti yako kama tarumbeta.

Watangazieni watu wangu uasi wao,

na kwa nyumba ya Yakobo dhambi zao.

Kwa maana kila siku hunitafuta,

wanaonekana kutaka kujua njia zangu,

kana kwamba walikuwa taifa linalotenda lililo sawa,

na ambalo halijaziacha amri za Mungu wake.

Hutaka kwangu maamuzi ya haki,

nao hutamani Mungu awakaribie.

Wao husema, ‘Mbona tumefunga, nawe hujaona?

Mbona tumejinyenyekeza, nawe huangalii?’

“Lakini katika siku ya kufunga kwenu, mnafanya mnavyotaka

na kuwadhulumu wafanyakazi wenu wote.

Kufunga kwenu huishia kwenye magomvi na mapigano,

na kupigana ninyi kwa ninyi kwa ngumi za uovu.

Hamwezi kufunga kama mnavyofanya leo

na kutazamia sauti zenu kusikiwa huko juu.

Je, hii ndiyo aina ya mfungo niliouchagua,

siku moja tu ya mtu kujinyenyekeza?

Je, ni kwa kuinamisha kichwa chini kama tete,

na kwa kujilaza juu ya gunia na majivu?

Je, huo ndio mnaouita mfungo,

siku iliyokubalika kwa Mwenyezi Mungu?

“Je, hii si ndiyo aina ya mfungo niliyoichagua:

kufungua minyororo ya udhalimu,

na kufungua kamba za nira,

kuwaweka huru waliodhulumiwa,

na kuvunja kila nira?

Je, sio kushirikiana chakula chako na wenye njaa

na kuwapatia maskini wasiokuwa na makao hifadhi,

unapomwona aliye uchi, umvike,

wala si kumkimbia mtu wa mwili wako

na damu yako mwenyewe?

Ndipo nuru yako itajitokeza kama mapambazuko

na uponyaji wako utatokea upesi;

ndipo haki yako itakapokutangulia mbele yako,

na utukufu wa Mwenyezi Mungu utakuwa mlinzi nyuma yako.

Ndipo utaita, naye Mwenyezi Mungu atajibu,

utalia kuomba msaada,

naye atasema: Mimi hapa.

“Ukiiondoa nira ya udhalimu,

na kunyoosha kidole na kuzungumza maovu,

nanyi mkimkunjulia mtu mwenye njaa nafsi zenu

na kutosheleza mahitaji ya waliodhulumiwa,

ndipo nuru yenu itang’aa gizani,

nao usiku wenu utakuwa kama adhuhuri.

Mwenyezi Mungu atakuongoza siku zote,

atayatosheleza mahitaji yako katika nchi kame,

naye ataitia nguvu mifupa yako.

Utakuwa kama bustani iliyonyweshwa vizuri,

kama chemchemi ambayo maji yake hayakauki kamwe.

Watu wako watajenga tena magofu ya zamani

na kuinua misingi ya kale;

utaitwa Mwenye Kukarabati Kuta Zilizobomoka,

Mwenye Kurejesha Barabara za Makao.

“Ukitunza miguu yako isivunje Sabato,

na kutokufanya kama vile upendavyo katika siku yangu takatifu,

ukiita Sabato siku ya furaha

na siku takatifu ya Mwenyezi Mungu ya kuheshimiwa,

kama utaiheshimu kwa kutoenenda

katika njia zako mwenyewe,

na kutokufanya yakupendezayo

au kusema maneno ya upuzi,

ndipo utakapojipatia furaha yako katika Mwenyezi Mungu,

nami nitakufanya upande juu ya miinuko ya nchi

na kusherehekea urithi wa Yakobo baba yako.”

Kinywa cha Mwenyezi Mungu kimenena haya.

Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu. Copyright © 2018, 2024 Biblica, Inc. Licensed under CC BY-SA 4.0. “Biblica” ni alama ya biashara iliyosajiliwa katika United States Patent and Trademark Office (ofisi ya hataza na alama za biashara Marekani) na shirika la Biblica, Inc. Source: eBible.org. Typeset from the source files; no intended changes to scripture wording. BibleKenya is not endorsed by the rights holder.

Full source notice & licence · CC BY-SA 4.0 · SourceEdition imported 2026-10-25.

BibleKenya

Reader settings

Theme
Font
Alignment
Reading width

Saved in this browser and used offline too. Press ? for keyboard shortcuts.