Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu
Isaya 4
Katika siku ile wanawake saba
watamshika mwanaume mmoja
wakisema, “Tutakula chakula chetu wenyewe
na kuvaa nguo zetu wenyewe,
ila wewe uturuhusu tu tuitwe kwa jina lako.
Utuondolee aibu yetu!”
Tawi la Mwenyezi Mungu
Katika siku ile Tawi la Mwenyezi Mungu litakuwa zuri na lenye utukufu, nalo tunda la nchi litakuwa fahari na utukufu wa wale Waisraeli watakaonusurika. Wale watakaoachwa Sayuni, watakaobaki Yerusalemu, wataitwa watakatifu, wale wote ambao wameorodheshwa miongoni mwa walio hai huko Yerusalemu. Bwana atausafisha uchafu wa wanawake wa Sayuni, atatakasa madoa ya damu kutoka Yerusalemu kwa Roho ya hukumu na Roho ya moto. Kisha Mwenyezi Mungu ataumba juu ya Mlima wote wa Sayuni, na juu ya wale wote wanaokusanyika hapo, wingu la moshi wakati wa mchana, na kung’aa kwa miali ya moto wakati wa usiku; nako juu ya huo utukufu wote kutatanda kifuniko cha ulinzi. Utakuwa sitara na kivuli kutokana na joto la mchana, na kuwa mahali pa kujificha kutokana na dhoruba na mvua.
Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu. Copyright © 2018, 2024 Biblica, Inc. Licensed under CC BY-SA 4.0. “Biblica” ni alama ya biashara iliyosajiliwa katika United States Patent and Trademark Office (ofisi ya hataza na alama za biashara Marekani) na shirika la Biblica, Inc. Source: eBible.org. Typeset from the source files; no intended changes to scripture wording. BibleKenya is not endorsed by the rights holder.
Full source notice & licence · CC BY-SA 4.0 · SourceEdition imported 2026-10-25.