Skip to content
BibleKenya

Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu

Isaya 13

Unabii dhidi ya Babeli

Neno la unabii kuhusu Babeli ambalo Isaya mwana wa Amozi aliliona:

Twekeni bendera juu ya mlima usio na kitu,

wapazieni sauti,

wapungieni mkono waingie

katika malango ya wenye heshima.

Nimewaamuru watakatifu wangu;

nimewaita mashujaa wangu waitimize hasira yangu:

wale wanaoshangilia ushindi wangu.

Sikilizeni kelele juu ya milima,

kama ile ya umati mkubwa wa watu!

Sikilizeni, makelele katika falme,

kama mataifa yanayokusanyika pamoja!

Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni anakusanya

jeshi kwa ajili ya vita.

Wanakuja kutoka nchi za mbali sana,

kutoka miisho ya mbingu,

Mwenyezi Mungu na silaha za ghadhabu yake,

kuangamiza nchi yote.

Ombolezeni, kwa maana siku ya Mwenyezi Mungu i karibu,

itakuja kama uharibifu kutoka kwa Mwenyezi1.

Kwa sababu ya hili, mikono yote italegea,

moyo wa kila mtu utayeyuka.

Hofu itawakamata,

uchungu na maumivu makali yatawashika,

watagaagaa kama mwanamke aliye na uchungu wa kuzaa.

Watatazamana kwa hofu kila mtu na mwenzake,

nyuso zao zikiwaka kama moto.

Tazameni, siku ya Mwenyezi Mungu inakuja,

siku katili, yenye ghadhabu na hasira kali,

kuifanya nchi kuwa ukiwa,

na kuwaangamiza wenye dhambi waliomo.

Nyota za mbinguni na makundi ya nyota

havitatoa mwanga wake.

Jua linalochomoza litatiwa giza

na mwezi hautatoa nuru yake.

Nitauadhibu ulimwengu kwa ajili ya uovu wake,

waovu kwa ajili ya dhambi zao.

Nitakomesha majivuno ya wenye kiburi,

na nitakishusha kiburi cha watu wakatili.

Nitawafanya wanadamu kuwa adimu kuliko dhahabu safi,

watakuwa wachache sana kuliko dhahabu ya Ofiri.

Kwa hiyo nitazifanya mbingu zitetemeke,

nayo dunia itatikisika kutoka mahali pake

katika ghadhabu ya Mwenyezi Mungu,

Mungu wa majeshi ya mbinguni,

katika siku ya hasira yake iwakayo.

Kama paa awindwaye,

kama kondoo wasio na mchungaji,

kila mmoja atarudi kwa watu wake mwenyewe,

kila mmoja atakimbilia nchi yake ya kuzaliwa.

Yeyote atakayetekwa atapasuliwa tumbo,

wote watakaokamatwa watauawa kwa upanga.

Watoto wao wachanga watavunjwa vipande vipande

mbele ya macho yao;

nyumba zao zitatekwa,

na wake zao watanajisiwa.

Tazama, nitawachochea Wamedi dhidi yao,

ambao hawajali fedha

wala hawafurahii dhahabu.

Mishale yao itawaangusha vijana,

hawatakuwa na huruma kwa watoto wachanga

wala hawataangalia watoto kwa huruma.

Babeli, johari ya falme,

utukufu wa kiburi cha Wababeli2,

utaangushwa na Mungu

kama Sodoma na Gomora.

Hautakaliwa na watu kamwe,

wala watu hawataishi humo kwa vizazi vyote.

Hakuna Mwarabu atakayepiga hema lake huko,

hakuna mchungaji atakayepumzisha makundi yake huko.

Lakini viumbe wa jangwani watalala huko,

mbweha watajaza nyumba zake,

bundi wataishi humo

nao mbuzi-mwitu watarukaruka humo.

Fisi watalia ndani ya ngome zake,

mbweha ndani ya majumba yake ya kifahari.

Wakati wake umewadia,

na siku zake hazitaongezwa.

Source notes (2)
  1. Footnote Mwenyezi hapa ina maana ya Shaddai kwa Kiebrania.
  2. Footnote yaani Wakaldayo

Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu. Copyright © 2018, 2024 Biblica, Inc. Licensed under CC BY-SA 4.0. “Biblica” ni alama ya biashara iliyosajiliwa katika United States Patent and Trademark Office (ofisi ya hataza na alama za biashara Marekani) na shirika la Biblica, Inc. Source: eBible.org. Typeset from the source files; no intended changes to scripture wording. BibleKenya is not endorsed by the rights holder.

Full source notice & licence · CC BY-SA 4.0 · SourceEdition imported 2026-10-25.

BibleKenya

Reader settings

Theme
Font
Alignment
Reading width

Saved in this browser and used offline too. Press ? for keyboard shortcuts.