Skip to content
BibleKenya

Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu

Waebrania 13

Huduma inayompendeza Mwenyezi Mungu

Endeleeni kupendana kama ndugu. Msisahau kuwakaribisha wageni, kwa kuwa kwa kufanya hivyo, watu wengine waliwakaribisha malaika pasipo kujua. Wakumbukeni wale waliofungwa gerezani kana kwamba ninyi mmefungwa pamoja nao. Pia wakumbukeni wale wanaotendewa vibaya, kana kwamba ni ninyi wenyewe mnateswa.

Ndoa na iheshimiwe na watu wote, nayo malazi yawe safi, kwa kuwa Mungu atawahukumu wazinzi na waasherati wote. Yalindeni maisha yenu msiwe na tabia ya kupenda fedha, bali mridhike na vile mlivyo navyo, kwa sababu Mungu amesema,

“Kamwe sitakuacha,

wala sitakupungukia.”

Kwa hiyo tunaweza kusema kwa ujasiri,

“Mwenyezi Mungu ni msaada wangu; sitaogopa.

Mwanadamu anaweza kunitenda nini?”

Wakumbukeni viongozi wenu, wale waliowaambia neno la Mungu. Angalieni matokeo ya mwenendo wa maisha yao mkaiige imani yao. Isa Al-Masihi ni yeye yule jana, leo na hata milele.

Msichukuliwe na kila aina ya mafundisho ya kigeni. Ni vyema mioyo yenu iimarishwe kwa neema, wala si kwa sheria kuhusu utaratibu wa vyakula, ambavyo havina faida kwa wale wanaozishika hizo sheria. Sisi tunayo madhabahu ambayo wale wanaohudumu katika hema hawana haki ya kula vile vitu vilivyowekwa juu yake.

Kuhani mkuu huchukua damu ya wanyama na kuiingiza Patakatifu pa Patakatifu, kama sadaka ya dhambi, lakini miili ya hao wanyama huteketezwa nje ya kambi. Vivyo hivyo, Isa naye aliteswa nje ya lango la mji ili awatakase watu kwa damu yake mwenyewe. Kwa hiyo, basi na tumwendee nje ya kambi, tukiichukua aibu aliyobeba. Kwa kuwa hapa hatuna mji udumuo, bali tunautafuta ule ujao.

Basi kupitia kwa Isa, tuzidi kumtolea Mungu dhabihu ya sifa, yaani matunda ya midomo inayolikiri Jina lake. Na msiache kutenda mema na kushirikiana vile vitu mlivyo navyo, kwa kuwa dhabihu kama hizo ndizo zinazompendeza Mungu.

Watiini viongozi wenu na kujinyenyekeza chini ya mamlaka yao. Kwa maana wao wanakesha kwa ajili yenu kama watu watakaopaswa kutoa maelezo. Watiini ili wafanye kazi yao kwa furaha, wala si kama mzigo, maana hiyo haitakuwa na faida kwenu.

Tuombeeni. Tuna hakika kuwa tunayo dhamiri safi na shauku ya kuishi kwa uadilifu kwa kila njia. Ninawasihi zaidi mniombee ili nipate kurudishwa kwenu upesi.

Maombi ya kuwatakia baraka

Basi Mungu wa amani, ambaye kwa damu ya agano la milele alimleta tena kutoka kwa wafu Bwana wetu Isa, yule Mchungaji Mkuu wa kondoo, awafanye ninyi wakamilifu mkiwa mmekamilishwa katika kila jambo jema ili mpate kutenda mapenzi yake, naye atende ndani yetu kile kinachompendeza machoni pake, kupitia kwa Isa Al-Masihi, ambaye utukufu una yeye milele na milele. Amen.

Maneno ya mwisho na salamu

Ndugu zangu, nawasihi mchukuliane na maneno yangu ya maonyo, kwa kuwa nimewaandikia waraka mfupi tu.

Nataka mjue kwamba ndugu yetu Timotheo amefunguliwa kutoka gerezani. Akifika mapema, nitakuja pamoja naye kuwaona.

Wasalimuni viongozi wenu wote na watakatifu wote. Wale wa kutoka Italia wanawasalimu.

Neema iwe nanyi nyote. Amen.

Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu. Copyright © 2018, 2024 Biblica, Inc. Licensed under CC BY-SA 4.0. “Biblica” ni alama ya biashara iliyosajiliwa katika United States Patent and Trademark Office (ofisi ya hataza na alama za biashara Marekani) na shirika la Biblica, Inc. Source: eBible.org. Typeset from the source files; no intended changes to scripture wording. BibleKenya is not endorsed by the rights holder.

Full source notice & licence · CC BY-SA 4.0 · SourceEdition imported 2026-10-25.

BibleKenya

Reader settings

Theme
Font
Alignment
Reading width

Saved in this browser and used offline too. Press ? for keyboard shortcuts.